_*• Kakonko yatoa tenda za Sh. 43 Milioni*_
Halmashauri zilizopo Mkoa wa Kigoma zimetoa zabuni za umma zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 500 kwa makundi maalum ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, hadi kufikia Septemba 7, 2026.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kati na Magharibi, Mhandisi Suma Atupele, amemweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Mwang’onda, alipotembelea Banda la Mamlaka hiyo lililokuwa katika Uwanja wa Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma.
Mhandisi Atupele alisema Mkoa huo umesajili makundi maalum 1,359 kwenye Mfumo wa NeST, idadi ambayo ni zaidi ya lengo la kusajili makundi 1,200.
“Hili ni ongezeko la makundi 159. Aidha, halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Kigoma kwa ujumla zimetoa tenda zenye thamani ya Sh. 543,746,734.30,” alisema Mhandisi Atupele.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Ndugu Mustapha S. Mtungwe, alimweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kuwa Halmashauri hiyo imesajili makundi maalum 153 na kutoa tenda zenye thamani ya Sh. 43,170,146.74.
Ndugu Mwang’onda alizipongeza halmashauri za Mkoa huo zilizofikia malengo ya usajili wa makundi maalum na kuzitaka kuhakikisha zinatoa tenda kwa makundi hayo kwa kuzingatia asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi.
Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa alitoa rai kwa viongozi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwasajili na kuwapa tenda vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru 2026 katika Wilaya ya Kakonko unafanyika katika Uwanja wa Mwenge, Kakonko.
