Featured Kitaifa

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU KUPITIA BOOST

Written by Alex Sonna

OWM-TAMISEMI,Mwanza

Katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026, Serikali imetoa jumla ya Shilingi Trilioni 5.4 kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika elimu ya awali, msingi na sekondari nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI anayeshughulikia TAMISEMI, Sospeter Mtwale, kwa niaba ya Katibu Mkuu Bw. Adolf Ndunguru, wakati akifunga mafunzo kwa Walimu Wakuu wa shule za msingi na elimu ya awali pamoja na Wenyeviti wa Kamati za Ujenzi na Miundombinu ya shule 287 kutoka mikoa tisa, yaliyotolewa kupitia Mradi wa BOOST.

Bw. Mtwale amesema uwekezaji huo umewezesha Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya shule, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni, nyumba za walimu, maabara, vyoo na miundombinu mingine muhimu inayochangia kuweka mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya miradi 1,608 imetekelezwa, ikiwemo miradi 1,265 katika shule za msingi na miradi 1,104 katika shule za sekondari, huku Serikali ikiendelea kuongeza uwekezaji katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa miundombinu ya elimu.

Aidha, amesema jumla ya vyumba vya madarasa 907 vimejengwa, ambapo 608 ni vya shule za msingi na 299 ni vya shule za sekondari, huku pia kukiwa na utekelezaji wa miradi ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni na maabara.

Bw.Mtwale amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa shule, kamati za ujenzi na miundombinu pamoja na jamii, na kwamba ni muhimu wahusika wote kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya miradi zinatumika kwa uadilifu na miradi inakamilishwa kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.

Amesema mafunzo hayo kwa walimu wakuu na wenyeviti wa kamati za ujenzi na miundombinu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwawezesha wasimamizi wa miradi kuwa na uelewa wa taratibu za usimamizi, ujenzi na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuhakikisha miradi ya BOOST inaleta matokeo yaliyokusudiwa.

About the author

Alex Sonna