Gifted Nature NGO ni shirika lisilo la kiserikali la Tanzania lililoanzishwa mwaka 2021 na Dr. Sophia Mfaume Kizigo, linalojikita katika kuiwezesha jamii, kulinda mazingira pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana ili waweze kuwa na maisha yenye tija na endelevu. Kupitia programu zinazolenga jamii, shirika linashughulikia changamoto za kijamii na kimazingira huku likihamasisha elimu, uongozi, ukuzaji wa ujuzi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika maendeleo.
Miongoni mwa mipango yake muhimu ni Mradi wa ‘Shujaa Path’ ulioanzishwa mwaka 2025, unaolenga hasa kuwawezesha wavulana na vijana wa kiume ambao mara nyingi hawapati uangalizi wa kutosha katika programu mbalimbali za maendeleo. Shujaa Path umeanzishwa kutokana na kutambua changamoto zinazowakabili wavulana, zikiwemo kuacha au kutoshiriki kikamilifu katika elimu, ukosefu wa malezi na ushauri wa kitaalamu, ukosefu wa ajira na fursa za kiuchumi, ushawishi hasi wa rika pamoja na ukosefu wa mazingira bora ya kukuza vipaji na uwezo wao.
Kupitia kaulimbiu “Every Boy, A Shujaa – Kila Kijana wa Kiume ni Shujaa,” Shujaa Path hailengi tu kutatua changamoto zinazowakabili wavulana, bali kuwasaidia kutambua thamani na uwezo wao, kujenga kujiamini, kuwa na maadili mema, kupata ujuzi wa maisha, ujasiriamali na ajira, pamoja na kuwa viongozi na raia wenye mchango chanya katika familia na jamii zao.
Gifted Nature NGO inaamini kuwa kumjenga kijana leo ni kuijenga jamii bora ya kesho. Kupitia ushirikiano na Serikali, shule, jamii, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari, shirika linalenga kuendeleza na kupanua Shujaa Path ili kuwafikia wavulana na vijana wengi zaidi Tanzania.
