Featured Kitaifa

NGASONGWA: FCC YAENDELEA KUPAMBANA NA BIDHAA BANDIA

Written by Alex Sonna

 

Na Mwandishi Wetu

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, ameanza ziara ya kikazi mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia na kukuza ushindani wa haki katika soko.

Katika ziara hiyo, iliyofanyika leo Agosti 12, 2026, Bi. Ngasongwa amekutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Balandya Elikana, ambapo wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia.

Akizungumza katika kikao hicho, Balandya amesema udhibiti wa bidhaa bandia ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa halali zinapata fursa sawa ya kushindana katika soko, hatua ambayo itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.

“Kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia kutasaidia kuwalinda wafanyabiashara wanaofuata sheria, kuongeza imani ya wananchi kwa bidhaa zinazouzwa sokoni na kuchochea ukuaji wa uchumi.”amesema Balandya

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema Tume itaendelea kuchukua hatua dhidi ya uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa bandia ili kuhakikisha bidhaa halali zinapata mazingira bora ya ushindani katika soko.

Bi.Ngasongwa amesema kuwa  hatua hizo ni sehemu ya jitihada za FCC za kulinda ushindani wa haki, kuwalinda wafanyabiashara wanaozingatia sheria na kuhakikisha shughuli za kibiashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

  

About the author

Alex Sonna