Baadhi ya wadau wakiwemo wawekezaji kutoka nchini Uholanzi na watendaji kutoka taasisi zinazojihusisha na uwekezaji hapa nchini,wakiwa katika majadiliano juu ya namna ya kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji hapa nchini.
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mh.Wiebe de Boer, akizungumza katika mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),Dk Samweli Gwamaka,akizungumza katika mdahalo wa wadau wa masuala ya uwekezaji kutoka Uholanzi na Serikali ya Tanzania.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya uwekezaji, Wizara ya Viwanda na Biashara ,Aristides Mbwasi,akifunga mkutano huo.
Mkurugenzi Idara ya Uhamasishaji uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Revocatus Rashel, akielezea fursa mpya za uwekezaji zilizopo nchini na maboresho yanayofanywa na Serikali katika kuboresha uwekezaji nchini Tanzania kwa wadau hao wa uwekezaji kutoka Uholanzi
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mjadala wakati wa mkutano huo
**
Serikali ya Uholanzi na taasisi zinazoshughulikia masuala ya uwekezaji na biashara Tanzania,wamekutana na wawekezaji,wafanyabiashara kutoka nchi hizo kujadili changamoto katika biashara na uwekezaji hapa nchini na namna ya kuzitatua.
Akizungumza jijini Arusha katika mkutano wa kujadili masuala ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer,alisema majadiliano hayo ni muhimu baina ya nchi hizo na yatawezesha kufungua fursa za uwekezaji hapa nchini na kuimarisha uchumi wa Tanzania.
Alisema kupitia majadiliano hayo yatatumika kama jukwaa la kujadili juhudi za pamoja za kukuza mazingira bora ya biashara na uwekezaji ili iweze kuwa kivutio zaidi cha uwekezaji chenye ushindani.
Alisema wameridhishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuondoa vikwazo mbalimbali katika sekta hiyo.
“Uhusiano baina ya Tanzania na Uholanzi ni mkubwa na unategemea zaidi ushirikiano endelevu wa biashara na tumekuwa mshirika mkubwa maendeleo wa Tanzania kwa muda mrefu na kampuni nyingi za Uholanzi zimefanya uwekezaji Tanzania,”alisema
Alisema kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kujadili changamoto za kibiashara na uwekezaji kwa wawekezaji kutoka Uholanzi ambao wanawekeza hapa nchini na namna ya kuzitatua kwa kushirikiana kwani biashara imekuwa kichocheo cha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
“Mazungumzo haya ni muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji wa Uholanzi nchini Tanzania kwani ni muhimu kutambua mashirika ya kimataifa yamewekeza kwa kiasi kikubwa na mchango wake utaharakisha maendeleo hapa nchini,”aliongeza
Akifunga majadiliano hayo Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisema Uholanzi ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya Dk Ashatu Kijaji ,Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya uwekezaji kutoka Wizara hiyo, alisema kupitia majadiliano hayo wadau na wawekezaji hao wameridhika na maboresho katika upatikanaji wa vibali vya kazi,uhamiaji,ambapo wanatumia mfumo mmoja.
Alisema wameweza kutoa mrejesho juu ya maboresho ambayo wamefanya ili kuwezesha uwekezaji na biashara nchini,kujadiliana nao kwani wanatambua unapotatua changamoto moja nyingine hujitokeza hivyo wamesikiliza changamoto nyingine mpya ambazo wanafikiri serikali ishughulike nazo.
“Lingine tunajadiliana kwa pamoja kuweka mikakati ya namna gani wanaweza kutatua hizo changamoto na mrejesho ambao tumeupata katika maajdiliano ya muda mfupi ni kwamba wameridhika wawekezaji hawa,”alisema
“Unajua wawekezaji kutoka Uholanzi ni moja ya kampuni kubwa nchini, nikiongelea mfano kwenye kilimo wanafanya vizuri sana kwenye kilimo sekta za maua, matunda na mbogamboga,”aliongeza
Mkurugenzi huyo alisema serikali iko mbioni kukamilisha mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kuwezesha wawekezaji nchini na kuwa kwa sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kina Kituo cha utoaji huduma za mahali pamoja ,ambapo taasisi 12 zinahudumia wawekezaji hapo katika ofisi moja na kurahisisha huduma.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji kutoka TIC,Revocatus Rashel,alisema kuhusu wasiwasi wa baadhi ya wawekezaji kuhusu upatikanaji wa vibali vya kazi,serikali imefanya marekebisho ya sheria kwenye sheria inayosimamia utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini ambapo imeongeza idadi kutoka tano hadi 10.
“Mwanzoni ilikuwa ni wageni watano kwa kila mradi tena kwa kipindi kifupi cha kuanzisha yaani kujenga mradi ambapo ni miaka mitatu kulingana na certificate ya TIC lakini kwa sasa sheria imebadilishwa hadi 10 na imeongeza muda ni kipindi chote cha mradi,”alisema na kuongeza
“Unapokuwa na mradi wako unapohitaji wataalam unaoona hawako nchini ambao ni muhimu na watakuja kujenga uwezo kwa wataalamu wetu wa ndani, unaweza kuleta hadi 10 na kibali kinatolewa kwa mfumo wa kimtandao,”
Mkurugenzi huyo alisema mkutano huo ni muhimu kwa Tanzania kwani Uholanzi ni nchi muhimu katika uwekezaji nchini na ni mojawapo ya nchi 10 zinazoongoza uwekezaji Tanzania.
“Kupitia mkutano huu TIC tumeweza kuwapa na kuwaonyesha fursa mpya zilizopo za uwekezaji nchini,kuwaeleza maboresho yanayofanywa na serikali katika kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini,”alisema
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),mkoa wa Arusha ,Eva Raphael, alisema wakati mwingine wadau siyo kwamba hawataki kufuata sheria bali ni uelewa na kuwa mamlaka hiyo inawasaidia kuzielewa na kuzifata.
“Sheria zipo za kodi na wanatakiwa kuzifuata lakini sisi kama mamlaka tunatakiwa kuwasaidia kuzielewa na kuzifuata kwa sababu wakati mwingine usipomsaidia mtu kufuata sheria inakuwa ni mzigo kwake,” alisema