Featured Kitaifa

WIZARA YA MADINI YAONGEZA NGUVU MADINI MKAKATI NA UONGEZAJI THAMANI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Wizara ya Madini Serikali imeendelea kuonyesha dhamira thabiti ya kuifanya sekta ya madini kuwa injini kuu ya uchumi kwa kuweka mkazo katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini muhimu na mkakati pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani wa rasilimali hizo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 27, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

 Waziri Mavunde amesema  kuwa madini mkakati kama lithium, graphite, nickel, cobalt na rare earth elements yana mchango mkubwa katika maendeleo ya teknolojia za kisasa, ikiwemo nishati safi. Alibainisha kuwa dunia inaelekea zaidi kwenye matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, jambo linaloongeza thamani ya madini hayo kimataifa.

Aidha  Serikali imepanga kuimarisha uwekezaji katika utafutaji na uchimbaji wa madini hayo ili kuongeza uzalishaji na mapato ya Taifa. Aidha, tafiti za soko zitafanyika ili kuyatafutia madini hayo masoko mapya duniani, sambamba na kurahisisha utoaji wa leseni kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo.

“Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na rasilimali hizi kwa kuongeza ajira, mapato na maendeleo ya viwanda,” amesisitiza Mhe.Mavunde

Katika hatua nyingine, Serikali imeweka mkakati wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji na usafishaji wa madini ili kuongeza thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi. Hatua hiyo inalenga kupunguza uuzaji wa madini ghafi na badala yake kuongeza mapato kupitia bidhaa zilizoongezwa thamani.

Eneo la Buzwagi, wilayani Kahama, limetengwa maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini, hatua inayotarajiwa kuvutia wawekezaji wakubwa na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo hayo na nchi kwa ujumla.

Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha viwanda vya usafishaji wa dhahabu vinapata ithibati ya kimataifa ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la dunia.

Katika kukuza sekta hiyo zaidi, Tanzania inatarajia kuandaa Mkutano wa saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini utakaofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2026. Mkutano huo utawakutanisha wataalamu, wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kujadili fursa na changamoto zilizopo.

About the author

Alex Sonna