Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeweka mikakati kabambe ya kuimarisha sekta ya madini katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikilenga kuongeza mapato ya ndani, kudhibiti upotevu wa rasilimali, na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa leo Aprili 27, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha bungeni vipaumbele vya Wizara ya Madini, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Serikali itaongeza nguvu katika ukusanyaji wa maduhuli kwa kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa shughuli za uchimbaji nchini. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania pamoja na wawekezaji kwa uwazi na ufanisi.
Katika mkakati huo, Wizara itaendelea kusimamia kwa karibu masoko na vituo vya ununuzi wa madini ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato. Aidha, juhudi zaidi zitaelekezwa katika usimamizi wa madini ya ujenzi, viwandani pamoja na soko la tanzanite na madini mengine ya vito ili kuongeza thamani na mapato yatokanayo na rasilimali hizo.
Serikali pia imejipanga kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Madini kwa kuchukua hatua kali dhidi ya utoroshaji wa madini na biashara haramu. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, teknolojia ya kisasa itatumika, ikiwemo matumizi ya vifaa maalum kama kofia zenye kamera kwa wakaguzi na wathaminishaji wa madini, hususan katika eneo la Mirerani, mkoani Manyara, ambako madini ya tanzanite hupatikana kwa wingi.
Kwa upande wa kukuza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa, Serikali imeweka mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika utafiti wa madini na ufunguzi wa migodi mipya. Vilevile, usimamizi wa migodi utaimarishwa ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka sambamba na kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Katika hatua nyingine, Serikali itasisitiza utekelezaji wa sera ya matumizi ya bidhaa na huduma za ndani (local content), kwa kuitaka migodi mikubwa kuajiri Watanzania na kununua bidhaa kutoka kwa wazalishaji wa ndani. Hatua hiyo inalenga kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja.
Aidha, mazingira ya uwekezaji yataendelea kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo muhimu. Serikali imesisitiza kuwa wawekezaji watakaopewa leseni za uchimbaji wanapaswa kuanza uzalishaji kwa wakati mara baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria.
Kwa ujumla, mwelekeo huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kusimamia rasilimali za madini kwa tija, uwazi na manufaa mapana kwa Taifa na wananchi wake.