Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AZINDUA AFISI YA UHAMIAJI WILAYA YA KATI UNGUJA

Written by Alex Sonna

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa Wakazi wa Dunga mkoa wa Kusini Unguja kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, katika kuhakikisha amani inaendelea kushamiri nchini.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar katika hafla iliyofanyika katika eneo Dunga. 

Amewasihi kushirikiana na Serikali kwa njia ya kutoa taarifa mbalimbali kuhusu wahamiaji haramu, watu wanaoishi nchini kinyume cha sheria, au wanaojihusisha na shughuli haramu zilizo kinyume na malengo ya ukaazi wao. Makamu wa Rais amesema amani na umoja ni Tunu za Taifa, ambayo kila mtanzania anapaswa kuilinda.  

 Makamu wa Rais amewasihi wananchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuiletea nchi maendeleo ili kwa pamoja kuweza kufikia malengo ya kuboresha maisha ya kila Mtanzania na kuiletea maendeleo nchi.

 Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Taasisi za Serikali kuendelea kuwaamini na kuwapa watanzania wazawa kazi za ujenzi ili waendelee kupata uwezo wa kiteknolojia na kifedha. 

Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya uhamiaji kwa kutoa kandarasi kwa mtanzania mzawa katika ujenzi wa jengo la Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati, Unguja.

 Aidha, Makamu wa Rais amesema Serikali imejikita katika kuimarisha huduma za uhamiaji kwa kuboresha vitendea kazi na miundombinu kwa ujumla. Ameongeza kwamba Ujenzi wa Afisi za Uhamiaji za Wilaya ni njia mojawapo ya jitihada za kufikia azma hiyo. 

Sambamba na uboreshwaji wa Miundombinu ya Majengo, Serikali imeweka mkazo katika utoaji wa Mafunzo kwa watumishi, kusimamia stahiki za Watumishi, na kufanya maboresho ya mara kwa mara ya Sheria na Kanuni za Uhamiaji nchini. 

Vilevile, Makamu wa Rais amesema huduma za Kiuhamiaji Zanzibar ni muhimu na ni chachu katika kukuza sekta ya biashara, uwekezaji na utalii, kwa kuzingatia ongezeko kubwa la Wageni wanaotembelea Zanzibar, hususan katika kipindi ambacho Serikali zote mbili zimejikita kukuza Sekta ya Utalii kufuatia uzinduzi wa Filamu maarufu ya Royal Tour.

Makamu wa Rais amesema Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyoongozwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume yana historia kubwa kwa Zanzibar na watu wake. 

Tangu wakati huo, Mapinduzi hayo yameijengea heshima kubwa Zanzibar na kuwapa Wazanzibari wigo mpana wa kufanya maamuzi kuhusu maisha yao wenyewe na kujiletea maendeleo.

 Amesema pia Muungano umeimarisha zaidi umoja, mshikamano na kudumisha amani na utulivu, na kuchochea maendeleo kwa wananchi wote. Amesema Baada ya Mapinduzi na Muungano, huduma mbalimbali za jamii kama vile afya na elimu zilifunguka kwa wananchi wote. 

Jengo hilo la Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati limegharimu shilingi bilioni 2.1.

About the author

Alex Sonna