Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 24 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imebainisha rasmi vipaumbele vya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiahidi mageuzi makubwa yatakayobadilisha sura ya utoaji haki nchini na kuimarisha mchango wa sekta ya sheria katika maendeleo ya Taifa.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 24 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.
Amesema Wizara itaendelea kuboresha huduma za kisheria ili ziendane na mipango ya kitaifa, kikanda na kimataifa, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa ufanisi.
Katika mpango huo, Serikali imeweka mkazo katika mageuzi ya kina ya mfumo wa kisheria, hususan katika maeneo ya haki jinai na madai, ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi. Hatua hii inalenga kuondoa mianya ya ucheleweshaji wa kesi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa haki.
Moja ya vipaumbele vikubwa ni ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya utoaji haki, ikiwa ni pamoja na mahakama na vituo vya huduma za kisheria, ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, hasa walioko maeneo ya vijijini.
Serikali pia imepanga kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya jinai na madai, pamoja na kuongeza nguvu katika huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wa kifedha hawakosi haki zao.
Katika kulinda misingi ya utawala bora, Wizara imeweka mkazo katika kuimarisha haki za binadamu, masuala ya kikatiba na utoaji wa elimu ya uraia, hatua inayotarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao.
Aidha, Serikali inalenga kuongeza uwezo wa wataalam wa sekta ya sheria kupitia mafunzo ya ubobezi, sambamba na kuboresha huduma za ufilisi na usimamizi wa mali za wadhamini ili kulinda maslahi ya wanufaika.
Katika hatua ya kipekee, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sekta ya sheria yamepewa kipaumbele, yakilenga kurahisisha uelewa wa sheria kwa wananchi wengi zaidi.
Vilevile, Wizara itaendelea kuimarisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kuharakisha upatikanaji wa haki.
Katika kulinda rasilimali za Taifa, Serikali imeweka mkazo katika ulinzi wa utajiri asili na maliasili, pamoja na kusimamia mikataba na uwekezaji ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanatangulizwa.
Mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha uwajibikaji ndani ya sekta ya sheria nayo yamepewa nafasi kubwa, sambamba na mageuzi ya kidigitali yatakayorahisisha utoaji wa huduma na kuongeza uwazi.
Hatua nyingine muhimu ni kuanzishwa kwa mifumo ya ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi, ili kuimarisha usalama wao na kuongeza ufanisi katika utoaji wa ushahidi.
Kwa upande wa uchumi, Wizara imepanga kufanya mageuzi ya sheria yatakayovutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku ikihakikisha mazingira ya biashara yanakuwa rafiki na yenye uhakika wa kisheria.
Aidha, usimamizi wa rasilimali watu katika mhimili wa Mahakama utaimarishwa kwa kuhakikisha ajira, uteuzi, nidhamu na maadili vinafuata misingi ya haki na uwajibikaji.
Katika kuhakikisha utekelezaji wenye tija, Wizara itaweka mkazo katika tafiti, mapitio na tathmini za sheria ili kuendana na malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Taifa.
Kwa ujumla, vipaumbele hivi vinaashiria dhamira ya Serikali ya kujenga sekta ya sheria iliyo imara, jumuishi na yenye mchango mkubwa katika ustawi wa Taifa sekta ambayo si tu inalinda haki, bali pia inasukuma mbele gurudumu la maendeleo kuelekea mwaka 2050.