| Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akipokea tuzo maaalum kutoka kwa Mlezi wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha Tanzania (Tanzania Women in Finance Association – TAWiFA) ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, kama Ishara ya kutambua mchango wake kwa Chama hicho, wakati alipofika kufungua Mkutano wa Tatu wa Wanawake katika Sekta ya Fedha (Women in Finance Conference 2026), katika Jengo la Papu Tower, jijini Arusha. |
Na. Joseph Mahumi, WF, Arusha
Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha juhudi za uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia sekta ya fedha, ikitambua kuwa eneo hilo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na endelevu nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Wanawake katika Sekta ya Fedha (Women in Finance Conference 2026), ulioandaliwa na Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha Tanzania (Tanzania Women in Finance Association- TAWiFA), katika Jengo la Papu Tower, jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, wanawake wana nafasi kubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, na Tafiti za mapato na matumizi ya kaya (HBS) zinaonesha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu kwa uwekezaji, biashara na kuchangia nguvukazi katika sekta mbalimbali za Uchumi ikiwemo kuendesha zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati nchini, hali inayoonesha wazi mchango wao katika uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa ndani.
“Wanawake ni mhimili mkuu wa uzalishaji hususan katika sekta ya kilimo na biashara. Hivyo, kuwawezesha kupitia sekta ya fedha ni hatua muhimu katika kujenga uchumi imara,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Mhe. Balozi alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imechukua hatua mbalimbali kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuboresha mazingira ya biashara na kuanzisha mifuko ya uwezeshaji kwa wanawake na vijana ambapo kati ya mwaka 2022 na 2025, zaidi ya wanawake milioni 1.3 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 748 kupitia mifuko hiyo, hatua iliyosaidia kuanzisha na kukuza biashara zao.
Aliongeza kuwa, sekta ya fedha ina nafasi ya kipekee katika kukuza shughuli za wanawake kiuchumi kupitia huduma za benki, bima, masoko ya mitaji na mifumo ya kidijitali, ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.
“Zaidi ya asilimia 60 ya watumiaji wa mikopo ya kidijitali ni wanawake, jambo hili linaloonesha namna wanavyonufaika na maendeleo ya teknolojia ya fedha katika kukuza biashara zao” aliongeza Balozi Omar.
Mhe. Balozi Omar, aliipongeza TAWiFA kwa mchango wake katika kuwainua wanawake kiuchumi, akibainisha kuwa zaidi ya wanawake 800 katika maeneo ya Dodoma na Zanzibar pamoja na 200 mkoani Arusha wamepata mafunzo ya elimu ya fedha kupitia programu mbalimbali za chama hicho.
Aidha alitoa wito TAWiFA na wadau wengine kuimarisha juhudi za kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya elimu ya fedha ili waweze kutumia ipasavyo huduma za kifedha, kama ambavyo kaulimbiu ya mkutano huo ikisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuwawezesha wanawake kama njia ya kujenga ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa Taifa.
Alitamatisha hotuba yake kwa kuzitaka taasisi za fedha kubuni bidhaa na huduma zinazozingatia mahitaji ya wanawake katika makundi mbalimbali, hususan maeneo ya vijijini, ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi rasmi.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu Zanzibar ambaye pia ni mlezi wa chama hicho, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, alitoa rai kwa wadau wote ikiwemo taasisi za fedha, watunga sera na washirika wa maendeleo, kuendelea kushirikiana katika kuweka mazingira wezeshi ambayo yatawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa uoande wake, imechukua hatua kadhaa za kuwawezesha wanawake kiuchumi na katika sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuanzisha program mbalimbali ikiemo kutoa mikopo na kuwajengea miundombinu ya masoko.
Kwa Upande wake Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha Tanzania-TAWiFA), Bi. Fikira Ntomola, alisema kuwa uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya fedha si suala la hiari bali ni mkakati wa msingi wa kukuza uchumi wa taifa na kuwa uwepo wa viongozi wa juu serikalini unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuifanya ajenda hiyo kuwa kipaumbele cha kitaifa.
Bi. Ntomola alibainisha kuwa TAWiFA imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuwawezesha wanawake, ikiwemo kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa zaidi ya wanawake wajasiriamali 800 kutoka Dodoma na Zanzibar, pamoja na zaidi ya 200 mkoani Arusha na kuanzisha programu ya uanagenzi inayolenga kuandaa viongozi wanawake wa baadaye katika sekta ya fedha, ambapo tayari kundi la kwanza la washiriki limeanza kunufaika.
Aliongeza kuwa hivi sasa pia wameanzisha Mfumo wa Uanachama wa TAWiFA utakaosaidia kujenga kanzidata ya kitaifa ya wanawake waliopo katika sekta ya fedha ili kurahisisha upatikanaji wao katika fursa za uongozi na maamuzi.
“Wadau wote tunapaswa kushirikiana ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya wanawake, kwa kuwa tunapowawezesha wanawake katika sekta ya fedha hatupanui tu wigo wa usawa, bali tunaimarisha uchumi mzima wa Taifa na mkutano huu uwe chachu ya mabadiliko kwa kuchochea hatua za vitendo zitakazofungua milango zaidi ya fursa kwa wanawake nchini” alisema Bi. Ntomola.
Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania – BOT, Bi. Sauda Msemo, alisema Ujumuishwaji wa wanawake katika ngazi za maamuzi unatoa fursa ya mabadiliko, Unarekebisha pengo la kimuundo (bridges structural inequities), na huonyesha ufanisi wa soko, na kushughulikia vikwazo vilivyopo upande wa watumiaji wa huduma kwa usahihi na umakini (addresses demand-side constraints with precision and empathy).
Bi. Msemo aliongeza kuwa Benki Kuu ilitoa maelekezo kuhakikisha kuwa walau theluthi moja ya viongozi kwenye menejimenti na bodi ni wanawake na kutoa muda wa miezi 36 kukamilisha utekelezaji wake kikamilifu ambapo hadi sasa, muelekeo unaridhisha.
Alisema kuwa hivi sasa kuna ongezeko la benki na taasisi za fedha zenye theluthi moja au zaidi ya viongozi wanawake kwenye bodi, huku ikishuhudia uandaaji wa mpango wa urithishaji wa madaraka (succession planning) kupitia programu mbalimbali za uongozi, kimalezi na ushauri (Leadership development programs, Mentorship and coaching) ili kuhakikisha uendelevu wa juhudi za ujumuishwaji wa viongozi wanawake.
“Juhudi hizi sio tu zinasaidia kuziba pengo la uongozi kijinsia, bali pia huhakikisha kuwa mitazamo ya kijinsia inazingatiwa katika muundo wa bidhaa, utawala, na ufanyaji maamuzi wa kimkakati, unaoathiri moja kwa moja matokeo ya ujumuishaji wa kifedha” alisema Bi. Msemo.




