Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), akiongoza kikao chake na Ujumbe wa Benki ya Standard Chartered, ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bw. Herman Kasekende (kushoto), ambapo walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Benki ya Standard Chartered, imeipongeza Tanzania baada ya Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na kufanya tathimini ya uwezo wa nchi kuyafikia masoko ya mitaji na dhamana ya kimataifa ya Moody’s Investors Limited, kuithibisha kuwa katika kiwango cha daraja la B1 na Mtazamo thabiti.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Bw. Herman Kasekende, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ambapo walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo, hususan ufadhili ya Reli ya Kisasa ya SGR.
Bw.Kasekende alisema kuwa Tanzania inafanya vizuri katika kusimamia uchumi wake ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha thamani ya sarafu yake, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na usimamizi thabiti wa deni lake la Taifa, ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Moody’s imeitathimini Tanzania kwa vigezo mbalimbali ambapo licha ya misukosuko kadhaa, umeiona nchi ikifanya maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.Mwaka 2023, Kampuni hiyo, kwa mara ya kwanza, iliifanyia Tathimini Tanzania na kuipa Alama B2 na baadae mwaka 2024, baada ya Serikali kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ikaipatia Tanzania alama B1, inayoiwezesha kuyafikia Masoko ya Mitaji na dhamana kwa gharama nafuu pamoja na Kujenga Imani ya kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka nje ya nchi.




