Featured Kitaifa

SERIKALI YATOA BILIONI 48.4 KUIMARISHA IAA KUPITIA MRADI WA HEET

Written by Alex Sonna

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka,akizungumza leo Februari 20,2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka,akizungumza leo Februari 20,2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kuimarisha elimu ya juu kama chachu ya mageuzi ya kiuchumi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 20, 2026, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema chuo hicho ni miongoni mwa taasisi zilizonufaika na mradi huo, kikipokea jumla ya shilingi 48,469,498,473/= kwa ajili ya kuboresha miundombinu, kufanya mapitio ya mitaala, kuimarisha teknolojia na kuwajengea uwezo watumishi wake. Mradi huo unafadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka World Bank.

“Kupitia HEET, IAA imefanikiwa kufanya mapitio ya mitaala 15 kwa gharama ya shilingi milioni 160, hatua inayolenga kuhakikisha kozi zinazotolewa zinaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi,” amesema Prof. Sedoyeka.

Aidha,amesema kuwa shilingi 446,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kuandaa mitaala mipya itakayozingatia ubunifu, teknolojia na fursa za kiuchumi zinazojitokeza kitaifa na kimataifa.

Katika kuimarisha ubora wa ufundishaji, wahadhiri 115 wa chuo hicho wanaendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi, hatua inayotarajiwa kuongeza wataalamu mahiri watakaosaidia kuzalisha wahitimu wenye ushindani.

Mapinduzi ya Kidijitali Chuoni

IAA imeanza kutekeleza mapinduzi ya kidijitali kwa kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 2 katika Madarasa Mahiri ya Akili Unde (AI Smart Classrooms). Madarasa hayo yana mifumo ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia inayotumia teknolojia ya hali ya juu, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi kwa njia ya kidijitali.

Sambamba na hilo, chuo kinaanzisha Kituo cha Kisasa cha Data kitakachosaidia kuhifadhi na kulinda taarifa muhimu za taasisi pamoja na kuimarisha usalama wa mifumo ya kidijitali.

Katika Kampasi ya Arusha, ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha TEHAMA (ICT Centre of Excellence) unaendelea kwa gharama ya shilingi 8,967,728,660.62. Kituo hicho kitakuwa kitovu cha ubunifu, tafiti na mafunzo ya teknolojia ya kisasa, kikilenga kuzalisha wataalamu wa TEHAMA watakaosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

Ujenzi wa Miundombinu ya Kisasa

Mbali na mageuzi ya kiteknolojia, IAA inaendelea na ujenzi wa majengo ya taaluma, hosteli na utawala katika kampasi zake zote kwa gharama ya shilingi 42,387,636,306/=.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Hosteli Kampasi ya Arusha – shilingi 11,481,644,308/=,Hosteli Kampasi ya Babati – shilingi 7,397,676,079/,Jengo la Makao Makuu – shilingi 13,899,164,512/,Jengo la Utawala Babati – shilingi 4,959,057,372/,Jengo la Taaluma Dodoma – shilingi 4,649,094,035/=

Amesema kuwa Kupitia HEET, pia wanajenga majengo ya taaluma katika Kampasi ya Babati (shilingi 13,928,815,627.80) na Songea (shilingi 18,648,258,369.77), hatua inayolenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuongeza udahili wa wanafunzi.

Ushirikiano na Sekta Binafsi

Katika kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya soko la ajira, IAA imesaini jumla ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) 23 na taasisi mbalimbali, zikiwemo CEOs Round Table. Ushirikiano huo unahusisha mafunzo kwa vitendo, tafiti shirikishi, mihadhara ya kitaaluma na ubadilishanaji wa maarifa kati ya chuo na sekta binafsi.

Manufaa kwa Taifa

Kwa mujibu wa  Prof.Sedoyeka, uwekezaji huu ni wa kimkakati katika kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na teknolojia.

“IAA haiwekezi tu katika majengo na teknolojia, bali inawekeza katika mustakabali wa vijana na taifa kwa ujumla,” amesema.

Kupitia Mradi wa HEET, IAA imejiweka katika nafasi ya kuwa taasisi kinara katika kuzalisha wataalamu wabunifu, wenye ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya kiuchumi nchini.

IAA Yapanua Miradi ya Maendeleo na Fursa za Vijana mwaka 2025/26

Amesema kuwa IAA  imeendelea kuimarisha sekta ya elimu ya juu kwa kuwekeza katika miundombinu, teknolojia na programu bunifu zinazolenga kuwajengea vijana ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira. 

 “IAA  itaendelea kuweka mkazo katika kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapatia elimu na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiri wengine katika maeneo ya mijini na vijijini.”amesema

Amesema  mkakati huo unalenga kuibua na kuendeleza vipaji, ubunifu na maarifa kwa vijana, kwa kuzingatia fursa zilizopo katika maeneo wanayoishi. Serikali imeeleza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya vijana waliopata mafunzo sahihi na yenye tija.

Kuongezeka kwa Kampasi na Kozi

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi, mwezi Agosti 2025 IAA ilifungua kampasi mpya mkoani Geita, na hivyo kufanya idadi ya kampasi kufikia sita ambazo ni Arusha, Babati (Manyara), Bukombe (Geita), Dar es Salaam, Dodoma na Songea (Ruvuma).

Kwa mwaka wa masomo 2025/2026, IAA inatoa jumla ya kozi 81 katika ngazi mbalimbali,Astashahada (Certificate) – kozi 20,Stashahada (Diploma) – kozi 19,Shahada (Bachelor Degree) – kozi 27 na Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) – kozi 15

Kozi za Uanagenzi Zaimarisha Ujuzi wa Vitendo

Katika kozi 27 za shahada ya kwanza, tatu zinatolewa kwa mfumo wa Uanagenzi (Apprenticeship) kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya benki, bima na utalii.

Kozi hizo ni Shahada ya Usimamizi wa Utalii na Ukarimu na Uanagenzi,Shahada ya Usimamizi wa Bima na Uanagenzi na Shahada ya Benki na Uanagenzi

Kupitia mfumo huu, wanafunzi hutumia nusu ya muda wao darasani na nusu nyingine katika maeneo ya kazi, wakijifunza kwa vitendo. Mfumo huu unawawezesha wahitimu kuajirika au kujiajiri wakiwa tayari na uzoefu wa kazi.

Kiatamizi Chawainua Vijana Wabunifu

Kupitia Kituo cha Uanzishaji Biashara (IAA Business Start Up Centre), zaidi ya vijana 8,600 wamefikiwa katika mwaka wa masomo uliopita. Kati yao, vijana 1,520 walibuni mawazo ya biashara na kuanzisha zaidi ya biashara 50, huku kampuni 12 zikisajiliwa rasmi.

Makampuni hayo yanajikita katika biashara, teknolojia, sanaa na uhifadhi wa mazingira, yakitoa ajira kwa wahitimu na vijana wengine.

About the author

Alex Sonna