Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATAKA MAJAJI NA MAHAKIMU KULINDA AMANI WAKATI WA KUTOA HAKI

Written by Alex Sonna

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kabla ya kufungua mkutano huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2026.

Na.Alex Sonna-DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka majaji na mahakimu kulinda amani, usalama na utulivu wa taifa wakati wa kutoa haki.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) ,Rais Samia amesema  ni muhimu kwa watoa haki kusimama kwenye mstari wa haki na kufanya maamuzi bila hofu, upendeleo, chuki au huba.

“Mie ningependa sana msimamie kiapo chenu pindi mnapoapa kuwa mtasimamia haki kwa kuzingatia sheria na maadili bila hofu, upendeleo, huba wala chuki. Hiki ndicho kiapo chenu mnapoapishwa,” amesema Rais Samia.

Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2025/2050 imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na utulivu. Ameongeza kuwa mahakama ina nafasi muhimu katika kujenga taifa lenye haki na utulivu.

“Dira hii ya 2050 inatambua kwamba utawala bora na utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo endelevu. Hali hii haiwezekani bila mahakama imara na ya kuaminika,” amesema Rais Samia, amebainisha hatua ambazo serikali imeanza kuchukua kujenga mahakama yenye heshima na yenye uwezo wa kutoa haki kwa wananchi.

Rais Samia pia amezungumzia changamoto za watumishi wa Mahakama zilizotolewa na Jaji Mkuu, George Masaju, na kuwataka kuwa wavumilivu. Amesisitiza kuwa mafanikio ya hatua za kuboresha mahakama yatahifadhiwa polepole na kwa umakini.

“Wakati mwingine mazingira ya kazi ni magumu na stahiki zao ni ndogo. Tujipime hapo. Hatusemi hatutazingatia maslahi yenu, bali twendeni polepole, hatua kwa hatua,” amesema

Aidha, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa uwazi, usimamizi wa haki na kufuata misingi ya kikatiba na sheria. Ameeleza kesi za ukiukaji wa haki ambazo hazijapatiwa suluhu zinaathiri imani ya wananchi kwa mahakama.

Kwa upande wake,Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, amethibitisha kuwa huduma za mahakama za wilaya zinapatikana sasa hivi nchini kote, isipokuwa wilaya ya Chamwino na Mkalama ambapo ujenzi unaendelea, na wilaya ya Ikungi ambapo ujenzi unaanza mwaka huu wa fedha.

“Pamoja na hayo Tanzania bara zipo mahakama za hakimu mkazi katika mikoa yote nchini na kwamba mhimili huo upo kwenye mchakato wa kubadilisha jina hilo badala ya kuziita mahakama ya hakimu mkazi iitwe mhakama za mkoa ili zisaidia kuhakikisha kesi zilizopo katika maeneo hayo.”amesema Jaji Masaju

Ameongeza kuwa katika mchakato huo wakubadilisha jina,wameshirikiana kwa karibu sana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia idara ya uandishi wa sheria ili kuandaa muswada.

Aidha Jaji Masaju ameeleza kuwa mchakato huo ukikamilika utakuwa na tija kwani kwa sasa wananchi wapo mbele ya muda ambao tayari wameshaanza kuiita Mahakama ya Mkoa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli Jijini Dodoma kwa ajili ya kufungua Mkutano wa Mkuu wa mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) tarehe 13 Januari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju kabla ya kufungua Mkutano wa Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kabla ya kufungua mkutano huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2026.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju,akizungumza wakati wa  Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika leo Januari 13,2026 jijini Dodoma.

Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Elimo Masawe,akizungumza wakati wa  Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika leo Januari 13,2026 jijini Dodoma.

Matukio mbalimbali katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amekaa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju, Viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) uliofanyika katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli, Jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2026.

About the author

Alex Sonna