Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, amewahidi kuwajengea Kijijj maalum kundi la Wanawake na Samia mkoa wa Dodoma, hatua itakayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Mhe. Mavunde ametoa ahadi hiyo leo, Januari 12, 2026 Jijini Dodoma, wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi awamu ya kwanza kwa kundi hilo la Wanawake na Samia waliohitimu mafunzo ya VETA, hatua inayolenga kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.
“Nitakwenda kumtafuta Mkurugenzi wa Jiji, kwakuwa mnafanya shughuli inayohitaji watu wengi inabidi tupate eneo mjini na huduma zenu mnazozifanya ziwe zinapatikana eneo moja”,amesema.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ili kutatua changamoto za kijamii, hivyo wanaamini mwanamke akiwezeshwa jamii imewezeshwa kwani hilo limedhirika baada ya muda mfupi waliopata mafunzo mambo yameanza kubadilika.
“Nataka niwaone wakina mama wa Dodoma kupitia taasisi hii ya Wanawake na Samia mnazichangamkia fursa mbalimbali zilizoko katika Jiji la Dodoma, nataka kwa nafasi yangu kama Mbunge wenu niwasimamie kwa dhati kabisa wakina mama fursa hizi zibaki hapa,”amesema.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi
Mwenyekiti wa Wanawake na Samia mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Madidi amemhakikishia Mhe. Mavunde kuwa mafunzo waliyoyapata takribani Wanawake 664, ni mafunzo yenye ujuzi na weledi wa juu.
Kwa upande wao, wanufaika wa vitendea kazi hivyo wameishukuru serikali na Mheshimiwa Mavunde kwa msaada huo, wakisema umefungua ukurasa mpya katika maisha yao na kuwaondolea changamoto ya kukosa vifaa vya kuanzia kazi baada ya mafunzo.
Mafunzo ya VETA yameendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwaandaa vijana na makundi maalum kwa ajira binafsi, sambamba na jitihada za serikali za kukuza uchumi jumuishi na kutoa fursa sawa kwa wote.
