Featured Kitaifa

BARRICK BUZWAGI YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI MIRADI YA KUSAIDIA JAMII NA YENYE KULETA MAENDELEO ENDELEVU

Written by Alex Sonna

 

 

Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, Shaban Mikongoti (aliyevaa suti ya bluu),akizungumza alipofanya ziara kwenye mradi ujenzi wa chujio la maji ya mvua linalojengwa katika Kata ya Mwendakulima unaotekelezwa kwa ufadhili wa Barrick Buzwagi kwa ushirikiano na Serikali.

 

Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, Shaban Mikongoti (aliyevaa suti ya bluu),akipata maelezo alipofanya ziara kwenye mradi ujenzi wa chujio la maji ya mvua linalojengwa katika Kata ya Mwendakulima unaotekelezwa kwa ufadhili wa Barrick Buzwagi kwa ushirikiano na Serikali.

 

 

Diwani wa Kata ya Mwendakulima ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, Shaban Mikongoti, ameupongeza mgodi wa Barrick Buzwagi kwa ufadhili wa miradi mikubwa kwenye jamii ambayo itaacha alama baada ya mgodi huo ambao uko katika mchakato wa kufungwa kuhitimisha zoezi hilo, ambayo itaendelea kunufaisha jamii, kuzalisha mapato ya Serikali na kupanua wigo wa ajira kwa vijana.

 
Mikongoti ametoa wito huo wakati wa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo moja ya mradi aliotembelea na kukagua ni ujenzi wa chujio la maji ya mvua linalojengwa katika Kata ya Mwendakulima, mradi unaotekelezwa kwa ufadhili wa Barrick Buzwagi kwa ushirikiano na Serikali.
 
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 wa kuvuna na kujenga miundombinu ya kusambaza maji ya mvua unalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Manispaa ya Kahama.
 
Mikongoti amesema ujenzi wa miundombinu hii inaojengwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo sio tu itaboresha huduma kwa wananchi bali pia itazalisha nafasi za ajira na ametoa rai kwa vijana kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na fursa za ajira zitakazopatikana hususani katika kongani ya kiuchumi ya Buzwagi na ametoa wito kwa wawekezaji kwenye kongani hiyo kuwapatia kipaumbele vijana wa Kahama ajira hususani zisizohitaji ujuzi zikijitokeza.
 
“Vijana na wananchi wa Kahama changamkieni fursa mbalimbali zilizopo katika kongani ya kiuchumi ya Buzwagi, Serikali imekusudia kupanua wigo wa ajira kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ili kujiletea maendeleo kupitia uwekezaji huu na tunawakaribisha wawekezaji kuendelea kuwekeza katika Manispaa yetu na Serikali tayari imeweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi”,amesema.
 
Mwakilishi wa Barrick Buzwagi kwenye ziara hiyo,Tito Jonathan akiongea kwa niaba ya Meneja wa ufungaji mgodi alisema dhamira ya kampuni ya Barrick inayoendeshashughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals ni kuunga mkono jitihada za serikali kuhakkisha wananchi wanapata maji safi na salama.
 
Ufanikishaji wa mradi huu ni moja ya utekelezaji wa mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick unaojumuisha ushirikiano na wadau na vipaumbele ambavyo vimelenga kufanikisha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyopo Jirani na migodi yake sambamba na kufanikisha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).
 
Akiongea wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi huu mwezi Agosti mwaka huu,wakati wa mbio za mwenge wilayani Kahama, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na usimamamizi wa mazingira kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Kahama,(KUWASA) Mhandisi Magige Marwa, alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwezi huu umelenga kuhudumia zaidi ya asilimia 66% ya wakazi waishio manispaa ya Kahama na una uwezo wa kuzalisha milioni 10 kwa siku.
 
Mhandisi Marwa alifafanua kwamba mradi huu wa chujio la maji ya mvua kwa asilimia 62% umefadhiliwa na mgodi wa Barrick Buzwagi na asilimia 38% umefadhiliwa na KUWASA kupitia Wizara ya maji .
 

 

About the author

Alex Sonna