Featured Kitaifa

KATAMBI ATAKA TAASISI ZA VIWANDA NA BIASHARA KUONGEZA NGUVU KATIKA TAFITI ZA TEKNOLOJIA

Written by Alex Sonna

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amezitaka taasisi zote chini ya wizara hiyo kuongeza msukumo katika kufanya tafiti, hususan zinazohusisha matumizi ya akili mnemba, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani, Katambi alisema dunia inaenda kwa kasi katika mabadiliko ya kiteknolojia, hivyo ni muhimu kwa taasisi hizo kuendana na mwelekeo huo ili kuongeza ufanisi na ushindani.

Alibainisha kuwa tafiti zinazofanywa zinapaswa kuelekezwa zaidi kwenye maeneo ya kipaumbele kama kilimo na mazao yake, biashara na sekta nyingine zenye mchango wa moja kwa moja kwa uchumi wa Mtanzania. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzifanyia kazi tafiti hizo badala ya kubaki kwenye makabrasha.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,Patrobas Katambi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani Tanzania (FCT), Jaji Rose Ebrahim, aliwakumbusha wafanyabiashara kuzingatia sheria za ushindani kwa kuepuka vitendo kama kupanga bei ambavyo vinaathiri mlaji na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Ushindani Tanzania (FCC), Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho ya mwaka huu yameambatana na maazimio kadhaa, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na mamlaka nyingine ili kuleta mazingira bora ya ukuaji wa uchumi.

Siku ya Ushindani Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Desemba, na kwa mwaka huu imebeba kaulimbiu isemayo: “Akili Mnembe, Walaji na Sera za Ushindani.”

About the author

Alex Sonna