Featured Kitaifa

WAZIRI AWESO AANZA NA DODOMA, BILIONI 62 KUTEKELEZA MIRADI YA MUDA MFUPI

Written by Alex Sonna

 

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameanza na mkakati mahsusi wa kuboresha huduma ya maji jijini Dodoma kwa kutekeleza miradi ya muda mfupi yenye thamani ya shilingi bilioni 62.

Amesema kuwa pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika Mkoa wa Dodoma, Wizara ya Maji imeweka mkakati kabambe wa muda mfupi, wa kati na mrefu ili kumaliza kabisa changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo ya pembezoni.

Amedokeza kuhusu hatua hiyo akiwa anazungumza na Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).

“Tutaanza na mpango wa muda mfupi kwa kutenga Sh. bilioni 62 za kutekeleza miradi ya haraka kama mkakati wetu wa awali kwa Jiji la Dodoma. Jiji la Dodoma ni makao makuu ya nchi ni wajibu wetu kuhakikisha huduma ya maji inakuwa bora, inayotabirika na endelevu”, Aweso amesema.

“Kama Waziri wa Maji niwahakikishie tutawekeza fedha za kutosha, nguvu na akili zetu zote kufanikisha lengo hili kwa maendeleo na ustawi wa Jiji la Dodoma na wakazi wake”, Aweso amesisitiza.

Kwa upande mwingine, Waziri Aweso amesema Wizara ya Maji itatoa kipaumbele kuimarisha eneo la utoaji huduma kwa wateja ili kumaliza kero na malalamiko ya wananchi kwa kusisitiza kuwa huduma zinazotolewa zinakuwa bora, za kuaminika na endelevu kwa kuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja.

“Kipaumbele chetu ni kusimamia kwa ukaribu eneo la utoaji wa huduma, kwetu mteja ni mfalme ni lazima apate huduma bora na endelevu. Tukihakikisha kero na malalamiko ya Watanzania yanapungua kama sio kuisha kabisa”, Aweso amesisitiza.

Amezitaka Mamlaka za Maji kutokuzoea kero za wananchi kwa kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zao pindi wanapozibaini au wanapopata taarifa, pamoja na kuacha utamaduni waburasimu kwa wateja.

Waziri Aweso amesema kuwa menejementi ni chombo cha uwajibikaji na kuilekeza Menejimenti ya DUWASA kuhakikisha taasisisi inatimiza malengo yake kwa ufanisi na kuitaka kuongeza kiwango cha uzalishaji maji ambacho kimefika lita milioni 88 kwenda hadi lita milioni 121 kwa siku pamoja na kuongeza muda wa upatikanaji wa huduma ya maji kuwa saa 24.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amehikiza watumishi wa DUWASA kuwathamini wateja wote kwa kuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja na kuhakikisha wanafuata Sheria, Taratibu na Kanuni katika majukumu yao. Pia, amewataka kupunguza changamoto ya upotevu wa maji, ambayo kwa sasa ni asilimia 32 ambayo ni kupoteza mapato na kuzorotesha huduma kwa wananchi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA amesema utendaji wa mamlaka umeendelea kuimarika, ikifanikiwa kuongeza makusanyo kutoka Sh. bilioni 1.5 hadi bilioni 2.8 kwa mwaka kiasi ambacho pamoja na majukumu mengine kinatumika kuimarisha huduma kwa wateja.

About the author

Alex Sonna