Meneja wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Bw. Dickson Gama, akiwasilisha mada kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha na usajili wa vikundi, katika siku ya pili ya semina ya waandishi wa habari za uchumi na biashara inayoendelea jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewakumbusha wananchi na viongozi wa vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) kuwa kuendesha shughuli za huduma ndogo za fedha bila kusajili vikundi hivyo ni kosa kisheria, na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka taratibu hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 20,2025 jijini Dodoma na Meneja wa Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Bw. Dickson Gama, wakati akiwasilisha mada kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha na usajili wa vikundi, katika siku ya pili ya semina ya waandishi wa habari za uchumi na biashara inayoendelea jijini Dodoma.
Semina hiyo, inayoratibiwa na BoT, imewaleta pamoja waandishi kutoka Zanzibar, Dodoma, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya shughuli za kifedha na usimamizi wa mifumo ya huduma ndogo za fedha nchini.
Bw. Gama amesema adhabu kwa vikundi vinavyoendesha VICOBA bila usajili iko bayana katika sheria.
“Kwa wale ambao wanaendesha VIKOBA bila kusajiliwa, ni kosa kisheria. Adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja hadi milioni 10, kifungo cha miaka miwili hadi mitano, au vyote kwa pamoja,” amesema Bw. Gama
Amebainisha kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu, jumla ya vikundi 70,800 vya kijamii vilikuwa vimesajiliwa nchini kupitia Wezesha Portal, jukwaa la kidijitali linalosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ambalo ndilo hutumika kupokea na kuchakata maombi ya usajili kabla ya hatua nyingine kuidhinishwa.
Aidha amefafanua kuwa usajili huo ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018, inayolenga kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo, kuhakikisha mazingira salama ya kifedha na kuchangia malengo ya Serikali ya kupanua upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi.
Bw. Gama amesema mfumo wa Wezesha Portal ni rahisi, hauna gharama na umeundwa kupunguza urasimu ili kuwawezesha wananchi kusajili vikundi vyao kwa ufanisi.
“Huduma ndogo za fedha zina mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kusaidia makundi maalum ambayo awali hayakuwa na upatikanaji wa huduma hizo, hivyo kupunguza umasikini,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, BoT imewataka viongozi wa vikundi hivyo kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa fedha na matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi na uaminifu katika kusimamia michango ya wanachama.
Benki hiyo imesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia ni kichocheo muhimu cha kuongeza tija na utendaji wa vikundi vya huduma ndogo za fedha katika shughuli za kiuchumi za wanachama wake.