Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameipa Wizara ya Viwanda na Biashara siku 180 kuandaa Sera ya Biashara Changa, hatua inayolenga kuweka mfumo madhubuti wa kuratibu na kukuza biashara hizo ili kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo Oktoba 19, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Wiki ya Biashara Changa Tanzania 2026.
Amesema Serikali inatambua mchango wa biashara changa katika kukuza uchumi na ndiyo maana imetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kusaidia ukuaji wake. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuwa na sera itakayoweka mwongozo wa uratibu na utekelezaji wa mipango ya kuendeleza biashara hizo.
“Natoa siku 180 kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa Sera ya Biashara Changa. Nawaahidi nitasimamia hilo kwa niaba ya Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa,” amesema Mhe. Ndejembi.
Aidha, amependekeza uratibu wa biashara changa, ambao kwa sasa unasimamiwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, uhamishiwe Wizara ya Viwanda na Biashara ili kurahisisha usimamizi wake, kwa kuwa biashara hizo zinapatikana katika sekta mbalimbali za uchumi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kutafuta jengo lisilotumika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanzisha eneo maalumu la biashara changa.
Amesema eneo hilo litatoa fursa kwa wajasiriamali kukutana na kubadilishana mawazo, huku likirahisisha upatikanaji wa huduma na kuwawezesha wadau wa maendeleo, wakiwemo taasisi za kifedha, kuwafikia na kuwasaidia wamiliki wa biashara hizo.
