Featured • Kitaifa

MKENDA CUP YAIBUA VIPAJI VYA SOKA ROMBO, WACHEZAJI KUNG’ARA KIMATAIFA

Written by Alex Sonna

 

Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema mashindano ya Mkenda Cup yameendelea kuwa chachu ya kuibua na kukuza vipaji vya soka kutoka Rombo, huku baadhi ya wachezaji walioanza kucheza mashindano hayo sasa wakicheza katika timu kubwa ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza jijini Dodoma Oktoba 17, 2026, Prof. Mkenda amesema mafanikio hayo yanaonekana kupitia wachezaji mbalimbali waliopitia Mkenda Cup na baadaye kupata nafasi ya kucheza katika ligi za ushindani, akimtaja Suleiman Mwalimu kuwa miongoni mwa mifano ya wachezaji walioanzia Rombo na kufanikiwa kufika katika hatua kubwa zaidi za soka.

Amesema Mwalimu aliwahi kucheza timu ya Kilamfua Mokala katika mashindano ya Mkenda Cup, akieleza kuwa licha ya timu hiyo kuwa na kiwango kizuri, ushindani mkubwa kutoka kwa timu nyingine za Rombo uliifanya ishindwe kutwaa ubingwa katika kipindi ambacho mchezaji huyo alikuwa akiichezea.

Prof. Mkenda amesema baada ya kuondoka Rombo, Mwalimu aliendelea kupanda katika ngazi za soka na kuchezea timu mbalimbali, ikiwemo Singida, kabla ya kwenda kucheza nje ya Tanzania na kufikia hatua ya kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa akiwa na Wydad Casablanca ya Morocco.

“Katoka Rombo pale, akaenda Singida, baadaye akaenda Wydad Casablanca na akaiongoza safu ya mashambulizi katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia. Hii inaonyesha namna vipaji vinavyoweza kutoka kwenye mashindano ya ndani na kufika kwenye kiwango cha kimataifa,” amesema Prof. Mkenda.

Amesema pamoja na Mwalimu, wapo wachezaji wengine walioibuliwa Rombo ambao sasa wanacheza katika timu mbalimbali za ligi za ushindani, akiwataka vijana kuendelea kutumia fursa zinazotolewa kupitia Mkenda Cup ili kuendeleza vipaji vyao.

Amesisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha Rombo inaendelea kuwa kituo muhimu cha kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kucheza katika timu kubwa nchini na hata nje ya Tanzania.

About the author

Alex Sonna