Na Hassan Kimweri, WAF – Addis Ababa
Tanzania imesisitiza umuhimu wa Afrika kuwa na sauti moja, uongozi madhubuti na uwakilishi wenye nguvu katika maamuzi ya afya duniani ili kuhakikisha maslahi na vipaumbele vya Bara hilo vinapewa uzito katika mchakato wa mageuzi ya Muundo wa Mfumo wa Afya Duniani (Global Health Architecture – GHA).
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema hayo leo Agosti 23, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia, alipomwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Kikao cha ‘African High-Level Ministerial Committee’ kuelekea Mkutano wa 76 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO AFRO RC76).
“Tanzania inaunga mkono kikamilifu mchakato wa mageuzi ya GHA na kuipongeza Africa CDC kwa kuteuliwa kuwa Taasisi ya kikanda ya afya katika mchakato huo, hatua hii ni fursa kwa Afrika kushiriki kikamilifu katika kuamua mwelekeo wa mfumo wa afya duniani,” amesema Dkt. Samizi
Akizungumzia umuhimu wa mageuzi hayo kwa wananchi, Dkt. Samizi amesema mfumo wa afya duniani unapaswa kuzingatia mahitaji halisi ya nchi, ikiwemo upatikanaji wa fedha, teknolojia na uwezo wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
“Dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha za afya, mabadiliko ya kijiografia na kisiasa pamoja na majadiliano kuhusu mkataba wa Kimataifa wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, upatikanaji wa vimelea na mgawanyo wa manufaa (PABS),” amesema Dkt. Samizi
Aidha, Dkt. Samizi amesema mfumo mpya wa afya duniani unapaswa kuwa na mgawanyo wa majukumu ulio wazi kati ya taasisi za kimataifa, kikanda na kitaifa, kupunguza urudiaji wa majukumu na kuhakikisha fedha zinaelekezwa katika vipaumbele vya nchi.
Kwa upande wa hatua zinazofuata, Dkt. Samizi amezihimiza nchi wanachama kushiriki kikamilifu katika mashauriano ya kila mwezi kuhusu mageuzi ya GHA, huku akipendekeza Afrika CDC na WHO AFRO ziwakutanishe Mawaziri wa Afya wa Afrika ifikapo Novemba 2026, baada ya kukamilika kwa rasimu ya kwanza ya ripoti ya “GHA Joint Task Force”, ili kupitia mapendekezo na kutoa mwongozo wa kisiasa.
Akihitimisha hotuba yake Dkt. Samizi amesema Tanzania inaendelea kutoa ushirikiano katika kujenga mfumo wa afya duniani wenye usawa, unaowajibika, unaoitikia mahitaji kwa wakati na unaozingatia changamoto za nchi zinazoendelea.
