Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 20,2026 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea kurahisisha upatikanaji wa fursa za zabuni za Serikali kwa kuanzisha programu ya simu janja ya NeST Tenderer, inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kushiriki katika ununuzi wa umma kwa urahisi zaidi.
Programu hiyo, inayopatikana kupitia Play Store na App Store, imeundwa kuwapeleka wananchi karibu na fursa za zabuni kwa kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Kielektroniki (NeST) kupitia simu zao.
Hayo yamesemwa leo Agosti 20,2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
BW.Simba, amesema NeST Tenderer inamwezesha mtumiaji kujisajili katika mfumo wa NeST, kutafuta na kuomba zabuni pamoja na kufuatilia taarifa za malipo bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi husika.
Amesema kuanzishwa kwa programu hiyo ni hatua muhimu katika kupunguza vikwazo vinavyoweza kuwazuia wananchi kushiriki kikamilifu katika fursa za ununuzi wa umma, hususan changamoto za umbali na gharama za kufuatilia zabuni.
“Lengo ni kuhakikisha fursa za zabuni za Serikali zinawafikia wananchi wengi zaidi, wakiwamo wale walioko mijini na vijijini,” amesema Simba.
Amesema matumizi ya NeST Tenderer yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kufuatilia zabuni kwa wakati, hatua inayoweza kuwawezesha kujiandaa na kushiriki katika ushindani wa zabuni kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Simba, mfumo huo pia unalenga kupunguza muda unaotumika katika kufuatilia michakato ya zabuni, kwa kuwa huduma muhimu zinapatikana kupitia simu janja bila ya mtumiaji kufika moja kwa moja katika ofisi za taasisi nunuzi.
Amesema upatikanaji wa huduma hizo kwa njia ya kidijitali ni sehemu ya juhudi za Serikali za kutumia teknolojia kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza uwazi na kupanua ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.
Simba amewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo kwa kujisajili katika mfumo wa NeST na kutumia programu ya NeST Tenderer kufuatilia fursa za zabuni zinazotangazwa na Serikali.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wa wazawa katika ununuzi wa umma na kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kunufaika na matumizi ya fedha za umma kupitia shughuli za biashara na utoaji wa huduma.