Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
WAKATI dunia ikishuhudia ongezeko la biashara ya zebaki kutoka tani 1,200 mwaka 2017 hadi tani 1,700 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 40, wadau wa mazingira wameonya kuwa matumizi ya kemikali hiyo katika uchimbaji mdogo wa dhahabu yanaendelea kuhatarisha afya za mamilioni ya watu, mazingira na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma kwenye warsha maalum wa Mradi wa marekebisho ya mkataba wa Zebaki na IPEN wenye lengo la kukomesha biashara ya zebaki duniani na kuweka tarehe ya kusitisha matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu (ASGM).
Mradi huo wa marekebisho ya Mkataba wa Zebaki wa IPEN unaotekelezwa na Taasisi ya AGENDA, ambayo ni mwanachama wa IPEN, unalenga kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Minamata kupitia kuongeza uelewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, mashirika ya kiraia, wabunge na vyombo vya habari.
Afisa Programu wa AGENDA, Angel Shaniva, amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi ya kukuza ushirikiano na kuongeza uelewa kwa wadau kuhusu masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi, elimu na jinsia.
Amesema lengo la mradi huo ni kuwashirikisha wadau wote muhimu wakiwemo Serikali, mashirika ya kiraia, wawakilishi wa vyombo vya habari na viongozi wa kisera ili kujadili hatua zilizopigwa na namna ya kuimarisha mapambano dhidi ya madhara ya zebaki.
Kwa mujibu wa AGENDA, marekebisho yanayopendekezwa katika Mkataba wa Minamata yanalenga mambo mawili makubwa; kwanza ni kukomesha biashara ya zebaki duniani na pili ni kuweka tarehe rasmi ya kusitisha matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu ifikapo mwaka 2032.
Kwa upande wa Mwasilishaji mwingine kutoka AGENDA, Clara Benjamin, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 153 wanachama wa Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki unaolenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya kemikali hiyo.
Amesema pamoja na hatua zilizopigwa chini ya mkataba huo, bado kuna changamoto ya kuendelea kwa biashara ya zebaki duniani na kutokuwepo kwa tarehe maalumu ya mwisho wa matumizi yake katika uchimbaji mdogo wa dhahabu.
Ameeleza kuwa sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu bado ndiyo inayochochea mahitaji makubwa ya zebaki duniani, ambapo hutumia zaidi ya tani 2,000 za kemikali hiyo kila mwaka bila dalili za kupungua.
“Uchimbaji mdogo wa dhahabu ndio unaotumia zebaki kwa kiwango kikubwa zaidi nchini Tanzania, huku matumizi hayo yakihusishwa na hatari kwa afya za wachimbaji, wanawake na watoto pamoja na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi,”amesema
Ametaja maeneo yenye matumizi makubwa ya zebaki kuwa ni pamoja na Geita, Shinyanga, Mbeya na Mara, ambapo wachimbaji hutumia kemikali hiyo katika kutenganisha dhahabu.
Amesema matumizi hayo husababisha uchafuzi wa ardhi, mito na samaki, huku pia yakihusishwa na madhara makubwa ya kiafya kama uharibifu wa mfumo wa fahamu na kuhatarisha usalama wa chakula.
Kwa upande wa mazingira, Afisa Mazingira Mkuu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Ahmad Hassan Mbwana, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza miradi inayolenga kupunguza matumizi yasiyo salama ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu.
Amesema kupitia programu hizo, elimu ya uhamasishaji imetolewa katika mikoa saba ikiwemo Mwanza na Geita, ambapo wachimbaji wadogo wameelimishwa kuhusu madhara ya matumizi ya zebaki na umuhimu wa kutumia njia salama zaidi katika uchakataji wa dhahabu.
Mbwana amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa sambamba na kusisitiza umuhimu wa kufanya tathmini za athari kwa mazingira kabla na wakati wa utekelezaji wa shughuli za uchimbaji.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu ya mazingira hauleti faida kwa uhifadhi pekee, bali pia unaongeza tija kiuchumi kwa wachimbaji kupitia matumizi ya teknolojia salama na usimamizi bora wa rasilimali.
Naye Mkaguzi wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), Thadei Mwasamila, amesema wachimbaji wadogo hujiona kama kundi lililoachwa nyuma, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa usalama katika maeneo ya uchimbaji.
Amesema ukaguzi wa mara kwa mara, kubaini vihatarishi na kuhakikisha wachimbaji wanazingatia viwango vya afya na usalama kazini ni hatua muhimu hasa katika maeneo yanayotumia kemikali hatarishi kama zebaki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NESODO, Alfred Lugela, amesema kupanda kwa bei ya dhahabu kumechangia matumizi holela ya zebaki katika shughuli za uchimbaji mdogo.
Amesema ikiwa bei ya zebaki itapanda kunaweza kuwafanya baadhi ya wachimbaji kuacha matumizi yake na kuelekea kutumia njia mbadala zilizo salama zaidi.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Mhandisi wa Migodi kutoka Wizara ya Madini, Yusuf Yusufu, amesema ni muhimu kuimarisha usimamizi wa shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu ili kuhakikisha wachimbaji wanafuata taratibu za kitaalamu na kutumia njia salama katika uzalishaji.
Amesema ushirikiano wa Serikali, wadau wa mazingira, wachimbaji na taasisi nyingine ni muhimu katika kujenga sekta ya madini yenye usalama na tija kwa wananchi.
Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Tawfiq Halfan, amesema masuala ya mazingira yanahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika bila kuhatarisha afya za wananchi na uharibifu wa mazingira.
Marekebisho ya Mkataba wa Minamata yanapendekeza pia Tanzania kuendelea kupanua matumizi ya teknolojia mbadala zisizotumia zebaki kama gravity concentration na borax, hatua inayolenga kulinda afya za wananchi, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini.

