Featured Kitaifa

COOP BANK YAJIVUNIA MAGEUZI, YATOA WITO WA UWEKEZAJI KUPITIA HISA

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

BENKI  ya Ushirika Tanzania (Cooperative Bank Tanzania Plc) imeendelea kuonyesha kasi ya ukuaji baada ya kuongeza mikopo kutoka Shilingi bilioni 14 mwaka 2024 hadi kufikia Shilingi bilioni 102 mwaka 2025, huku amana zikipanda kutoka Shilingi bilioni 15 hadi Shilingi bilioni 114, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa shughuli zake za kifedha na huduma kwa wateja.

Mafanikio hayo yameelezwa katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika Julai 31, 2026 jijini Dodoma, uliowakutanisha wanahisa, Bodi ya Wakurugenzi, viongozi wa benki na wadau mbalimbali kujadili utendaji wa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025 pamoja na mipango ya maendeleo ya taasisi hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank Tanzania Plc, Godfrey Ng’urah, amesema mwaka 2025 ulikuwa wa mageuzi makubwa yaliyoifanya benki hiyo kupanua huduma zake kwa wanachama wa vyama vya ushirika, wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara, wajasiriamali na makundi mengine ya wananchi.

Amesema pamoja na ongezeko la mikopo na amana, mtaji wa fedha za wanahisa umeongezeka kutoka Shilingi bilioni 27 wakati wa kuunganishwa kwa benki mbili zilizounda Coop Bank hadi kufikia Shilingi bilioni 42.

  “Benki hiyo pia imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya kidigitali kwa kuzindua huduma za Kopo Wakala, Kopo Pesa na COÖP Net, ambazo zimeongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za kifedha.”amesema Bw.Ng’urah

Amefafanua kuwa kupitia huduma ya Kopo Pesa, wateja wanaweza kufanya miamala mbalimbali kwa kutumia simu za mkononi ikiwemo kulipia LUKU, maji, umeme, ving’amuzi vya DSTV pamoja na kutuma na kupokea fedha kwa urahisi.

Aidha, amesema mfumo wa COÖP Net umeziwezesha taasisi na vyama vikuu vya ushirika kufanya malipo makubwa kwa wakati mmoja, ikiwemo mishahara na malipo kwa wanachama zaidi ya 3,000.

“Ni mwaka mkubwa, ni mwaka wa mageuzi, ni mwaka wa mafanikio. Tumejenga miundombinu imara na ya msingi kuhakikisha tunajenga benki kwa siku zijazo,” amesema Ng’urah.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amewataka wanahisa na wananchi kutumia fursa ya kuwekeza katika benki hiyo ili kuongeza nguvu ya mtaji na kuiwezesha kukua zaidi.

Amesema wakati wa uzinduzi wa benki hiyo hisa zilizoidhinishwa zilifikia Shilingi bilioni 58, huku akibainisha kuwa baada ya hatua hiyo kukamilika kutakuwepo na awamu nyingine ya kuongeza mtaji kupitia hisa mpya.

Dkt. Ndiege amesema fursa ya umiliki wa benki hiyo ipo kwa makundi mbalimbali kupitia vyama vya ushirika, ikiwemo waandishi wa habari, wavuvi, vijana na waendesha bodaboda.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Coop Bank imeonyesha mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake na ina uwezo wa kuwa miongoni mwa benki zinazoongoza kwa kasi ya ukuaji nchini.

“Ni muda mfupi tangu benki hii ianze, lakini tayari tunaona mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma. Sisi ambao tumefungua akaunti hapa tunashuhudia ubora wa huduma zake,” amesema  Senyamule.

Akichangia mjadala huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA SACCOS, Mbogo Kerenge, amesema ukuaji wa Coop Bank utaongeza uwezo wa vyama vya ushirika kupata mikopo kwa urahisi kutokana na kuimarika kwa ukwasi wa benki.

Amesisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kuunganisha nguvu kwa kuwekeza katika benki hiyo ili kuijenga iwe taasisi kubwa ya kifedha, akitoa mfano wa Benki ya Ushirika ya Kenya ambayo imefanikiwa kuwa miongoni mwa benki kubwa nchini humo kutokana na ushiriki mkubwa wa wanachama wa ushirika.

     

About the author

Alex Sonna