Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 18,2026 jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa Ebola na hatua zinazochukuliwa kuimarisha utayari wa taifa.
Na Edward Winchislaus
Serikali imeendelea kuimarisha hatua za kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini huku ikithibitisha kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa aliyegundulika Tanzania, licha ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 18,2026 jijini Dodoma , Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema mifumo ya ufuatiliaji, utambuzi na udhibiti wa ugonjwa huo imeimarishwa ili kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania unaendelea kulindwa wakati wote.
Amesema Serikali ilichukua hatua za mapema mara baada ya kutangazwa kwa mlipuko huo katika nchi jirani, ikiwemo kutoa Mwongozo wa Wasafiri Na. 17 wa Mei 19, 2026, unaobainisha tahadhari na masharti ya kiafya kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.
“Tunaendelea kuwafahamisha wananchi kuwa hadi sasa nchi yetu haina mgonjwa wa Ebola na hali ya usalama wa afya nchini iko vizuri. Serikali imejipanga kikamilifu kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote la ugonjwa huo,” amesema Mchengerwa.
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi za ugonjwa huo katika jamii pamoja na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege, kwa lengo la kubaini mapema viashiria vya maambukizi.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, jumla ya tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa nchini, ambapo wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi na kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo. Hata hivyo, matokeo yote yalionyesha kuwa hawakuwa na maambukizi ya Ebola.
Aidha, amesema Serikali imehakikisha upatikanaji wa vifaa kinga, vifaa tiba na dawa muhimu kwa wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Pia, maabara mbili za kupima Ebola zimesimikwa katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili kusogeza huduma za uchunguzi karibu zaidi na wananchi.
Katika hatua nyingine, jumla ya wahudumu wa afya 45,000 wamefikiwa kupitia mafunzo ya ana kwa ana na ya mtandaoni kuhusu namna ya kutambua, kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo. Elimu ya kinga dhidi ya Ebola pia imeendelea kutolewa kwa wasafiri, jamii za mipakani na wananchi kwa ujumla.
“Kuanzia kutangazwa kwa mlipuko huo, jumla ya vyombo vya usafiri 101,302 vimekaguliwa na wasafiri 164,652 wamechunguzwa katika mipaka, viwanja vya ndege na bandari. Zoezi hili linaendelea kuimarishwa katika maeneo yote ya kuingilia nchini,” amesema.
Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kutoa taarifa mapema kuhusu wahisiwa wa ugonjwa huo na kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa.
Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi unabaki kuwa nguzo muhimu katika kuilinda Tanzania dhidi ya tishio la Ebola na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama kiafya.