Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula yaliyosafishwa yanayoingizwa kutoka nje hadi asilimia 35 au Dola za Marekani 300 kwa tani, katika jitihada za kulinda viwanda vya ndani na kuharakisha azma ya nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta ya kula.
Akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.
Amesema sekta ya mafuta ya kula ina mchango mkubwa katika kukuza ajira, kuongeza mapato ya serikali na kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, hivyo serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wazalishaji wa mbegu za mafuta na viwanda vya uchakataji.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali itaendelea kutoza ushuru wa forodha kwa mafuta ghafi ya kula yanayoagizwa kutoka nje kwa kiwango cha chini ili kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata malighafi kwa gharama nafuu na kuongeza uzalishaji.
Aidha, serikali imependekeza kuanzishwa kwa ushuru wa mauzo ya nje kwa mbegu za mafuta ghafi, hatua inayolenga kuhamasisha uchakataji wa ndani badala ya kusafirisha malighafi bila kuongeza thamani.
“Lengo ni kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanachakatwa hapa hapa nchini ili kuongeza ajira, mapato na kukuza viwanda vya ndani,” amesema Waziri Omar.
Serikali imeeleza kuwa hatua hizo za kikodi ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuifanya Tanzania kujitosheleza kwa mafuta ya kula yanayozalishwa ndani ya nchi, huku ikiongeza ushindani wa viwanda vya ndani katika soko la kikanda na kimataifa.