Wizara ya Uchukuzi imeweka vipaumbele vinane katika mwaka wa fedha 2026/27, vikiwa na lengo la kuimarisha miundombinu na huduma za sekta ya uchukuzi nchini, ikiwemo reli, bandari, anga na mafunzo.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Mei 13, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema vipaumbele hivyo vitazingatia miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na uboreshaji wa huduma za uchukuzi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuendelea na ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR Tanzania, pamoja na ukarabati na uboreshaji wa reli za MGR na Tazara.
Aidha, wizara hiyo itaendelea kuboresha miundombinu na huduma katika sekta ya bandari, kuimarisha usafiri wa anga, pamoja na ujenzi na ukarabati wa meli nchini.
Vipaumbele vingine ni kuboresha huduma za hali ya hewa, kuimarisha udhibiti, ubora na usalama wa huduma za uchukuzi, pamoja na kuendeleza uboreshaji wa vyuo vya mafunzo vya sekta hiyo ili kuongeza ufanisi na ujuzi kwa watendaji wake.