Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha kundi la Wanawake wenye Ulemavu, Nassriya Nassir Ali,ameomba Serikali kujenga shule jumuishi katika kila Mkoa ili kupunguza changamoto kwa watoto wenye ulemavu kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata elimu maalumu.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia bungeni Dodoma, Mhe.amesema watoto wengi wenye ulemavu wanapata wakati mgumu kupata huduma za elimu karibu na maeneo wanayoishi, akitolea mfano maisha yake binafsi ambapo alilazimika kutoka Zanzibar kuja kusoma Tanzania Bara.
Amesema pamoja na ujenzi wa shule hizo, Serikali inapaswa kuhakikisha lugha ya alama inafundishwa kama somo rasmi kuanzia shule za msingi ili kuongeza ujumuishaji katika mfumo wa elimu.
Pia ameomba kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Elimu na wadau wa elimu maalumu pamoja na vyama vya watu wenye ulemavu wakati wa kuandaa mitaala, miongozo na sera mbalimbali zinazohusu elimu.
Mbunge huyo amesema watu wenye ulemavu, hususan wenye uziwi, wanakabiliwa na changamoto kubwa katika masomo kutokana na mazingira ya ujifunzaji kutokuwa rafiki, hali inayosababisha baadhi yao kutumia muda mrefu zaidi kumaliza masomo.
Aidha, ameomba Serikali kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza walimu wa elimu maalumu na kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanajumuishwa katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kupata huduma muhimu za matibabu.
Katika hatua nyingine, amesema kuna umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za watoto wenye ulemavu na kuhakikisha vifaa vinavyotolewa vinafika kwa walengwa kwa mgawanyo unaozingatia mahitaji halisi.
Ameitaka pia Wizara ya Elimu kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya elimu maalumu akisema hali ya huduma kwa watu wenye ulemavu Zanzibar bado ni ngumu na inahitaji maboresho makubwa.