Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Mbunge wa Viti Maalum, Stella Ikupa (CCM) ameshauri Serikali kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watu wenye ulemavu kwa mfumo wa ruzuku ili kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi kutokana na mazingira yao.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu bungeni, Ikupa amepongeza maboresho ya sekta ya elimu yanayoendelea kufanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo ongezeko la shule pamoja na walimu wa elimu maalumu nchini.
Mbunge huyo ameikumbusha Serikali kuhusu upungufu wa bajeti kwa walimu wenye mahitaji maalumu waliopo kazini, akisema Kamati ya Bunge tayari imeshauri fedha zitengwe na yeye anaunga mkono hatua hiyo.
Amesema kuna umuhimu kwa walimu wote nchini kupewa mafunzo ya elimu maalumu ili kurahisisha ujumuishaji wa wanafunzi wenye ulemavu katika mfumo wa elimu.
Aidha, ameshauri shule za mabweni zinazohudumia wanafunzi wenye ulemavu kuwa na wasaidizi maalumu watakaosaidia kuwahudumia wanafunzi hao ili waweze kujifunza katika mazingira rafiki na salama.
Ikupa pia amesisitiza umuhimu wa lugha ya alama kuingizwa rasmi katika mitaala ya elimu akisema hatua hiyo itasaidia Watanzania wengi kuweza kuwasiliana na watu wenye uziwi kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, amependekeza kuanzishwa kwa Bodi au Mamlaka ya Elimu Jumuishi ili kusimamia masuala ya elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu, akidai kuwa mfumo wa sasa wa kitengo haujafanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa.