Featured Kitaifa

KIHONGOSI AMTAKA HECHE  KUJIELIMISHA KABLA YA KUZUNGUMZA MASUALA YA UCHUMI

Written by Alex Sonna

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi,akizungumza na waandishi wa habari  leo Aprili 7,2026 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la chama kuhusu kupanda kwa bei za mafuta na Gharama za maisha nchini.

….

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi,amesema kuwa changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ni ya kidunia na si ya Tanzania pekee, hivyo haipaswi kuingizwa katika mjadala wa kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 7, 2026 jijini Dodoma,Kihongosi amesema kuwa nchi nyingi duniani, zikiwemo zile zenye uchumi mkubwa, zimeathirika na hali hiyo na zimepitia wakati mgumu kutokana na kupanda kwa bei za mafuta.

Amesisitiza kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo, ni muhimu kuwepo kwa ukweli na mshikamano wa kitaifa, badala ya kubeba masuala ya kisiasa yanayoweza kupotosha wananchi.

Aidha, Kihongosi amemkosoa mmoja wa viongozi wa kisiasa kwa kutoa kauli kuhusu suala hilo bila kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya uchumi. Alimtaka kujielimisha zaidi kabla ya kuzungumzia mambo nyeti yanayohusu maisha ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Kihongosi alizungumzia kuhusu John Heche, akimtaka kutumia zaidi viongozi wenye uelewa wa masuala ya uchumi ndani ya chama chake, ikiwemo Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili kuepuka upotoshaji wa taarifa kwa umma.

Kihongosi aliongeza kuwa Watanzania wanatambua kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni changamoto ya kimataifa, na akasisitiza umuhimu wa nchi kuungana katika kutafuta suluhisho, kama ilivyofanyika wakati wa janga la COVID-19.

Aidha, alisisitiza kuwa mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi ni msingi muhimu wa kukabiliana na changamoto hizi kwa pamoja.

Pia Kihongosi ametoa wito kwa watanzania kudumisha mshikamano, umoja na upendo ili taifa liweze kupita katika kipindi hiki kigumu bila kuathiri ustawi wa wananchi.

About the author

Alex Sonna