Featured Kitaifa

CCM YAIAGIZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA ZA HARAKA KUKABILIANA NA ONGEZEKO LA BEI ZA MAFUTA

Written by Alex Sonna

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi,akizungumza na waandishi wa habari  leo Aprili 7,2026 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la chama kuhusu kupanda kwa bei za mafuta na Gharama za maisha nchini.

Na Alex Sonna, Mzalendo Blog – Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiagiza Serikali kuendelea kuchukua hatua mahsusi kukabiliana na ongezeko la bei za mafuta nchini, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro unaoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Hayo yamesemwa leo, Aprili 7, 2026, jijini Dodoma, na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, wakati akitoa tamko la chama kuhusu kupanda kwa bei za mafuta na Gharama za maisha nchini.

Kihongosi amesema kuwa CCM, kupitia Serikali yake, imeanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za Mafuta, ambao uko katika hatua za mwisho za maandalizi. Mfuko huo unalenga kupunguza makali ya bei za mafuta pale zinapopanda kwa kiwango kikubwa.

“Serikali inaendelea na mpango wa kuanzisha hifadhi ya mafuta ya kimkakati ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa wa uhakika hata wakati wa changamoto. Sambamba na hilo, ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta unaendelea, hatua itakayosaidia nchi kupata mafuta kwa bei nafuu na kuimarisha biashara ya nishati,” amesema Kihongosi.

Aidha, maboresho yanafanyika katika mfumo wa uagizaji wa mafuta kupitia ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) ili kupunguza gharama zisizo za lazima, ikiwemo zile zinazohusiana na meli kusubiri kupakua mafuta. Hatua hii inalenga kuongeza uwazi na ufanisi katika sekta ya mafuta.

Vilevile, Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) limeongezewa uwezo wa kuagiza mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji bila kupitia madalali, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama na bei kwa mtumiaji wa mwisho. Taasisi nyingine kama EWURA na PBPA nazo zinaimarishwa ili kuhakikisha ununuzi wa mafuta unafanyika kwa gharama nafuu zaidi.

Kihongosi amesema kuwa katika mkakati wa muda mrefu, CCM imeweka mkazo katika kuwekeza kwenye nishati mbadala na usafiri wa umma wa kisasa, ikiwemo matumizi ya gesi asilia (CNG) na magari ya umeme. Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa mafuta, gharama za usafiri na matumizi ya fedha za kigeni.

“CCM imesisitiza umuhimu wa kujenga uchumi wa uzalishaji unaolenga kuuza nje, pamoja na kupitia upya tozo na kodi kwenye mafuta ili kupunguza gharama kwa wananchi. Licha ya changamoto hii kuwa ya kimataifa, tuna imani kuwa chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, nchi itaweza kuvuka kipindi hiki na kujenga uchumi imara zaidi,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa CCM itaendelea kuisimamia Serikali kwa karibu ili kuhakikisha hatua zote zinazochukuliwa zinalenga kulinda maslahi ya wananchi na ustawi wa Taifa kwa ujumla.

About the author

Alex Sonna