Katibu Mkuu (Mipango) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, amefungua mkutano wa kitaifa unaowakutanisha taasisi za utafiti kujadili namna ya kuoanisha utafiti na mchakato wa upangaji wa maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo Machi 23, 2026 jijini Dodoma katika ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Kida amesema Tanzania ipo katika hatua muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kujenga uchumi wa trilioni moja pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi.
Amesema dira hiyo inalenga pia kutokomeza umasikini uliokithiri, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, pamoja na vifo vya watoto wachanga ifikapo mwaka 2050.
“Tutahakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayebaki katika umasikini uliokithiri, huku tukiboresha huduma muhimu za kijamii kama afya na elimu,” amesema Dkt. Kida.
Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utaendeshwa kupitia mipango ya muda mrefu itakayogawanywa katika vipindi vya miaka mitano mitano, huku kila mwaka ukiwa na mpango mahsusi wa utekelezaji wenye vipaumbele vya kitaifa.
“Tume ya Taifa ya Mipango itaendelea kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya uchumi na maendeleo, na itasimamia pamoja na kuratibu utekelezaji wa mipango hiyo,” ameongeza.
Akizungumzia nafasi ya utafiti, Dkt. Kida amesisitiza kuwa tafiti za kiuchumi na kijamii ni nyenzo muhimu katika kubuni sera bora, kuboresha utekelezaji wa mipango, na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
“Ni muhimu kuwa na mwongozo madhubuti wa tafiti unaozingatia vipaumbele vya taifa ili kuhakikisha matokeo yake yanatatua changamoto halisi za wananchi,” amesema.
Katika hatua ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa utafiti, Dkt. Kida ameeleza kuwa Tume ya Mipango inapanga kuanzisha mfumo wa kidijitali (portal) wa kuhifadhi na kusambaza tafiti zote zinazofanyika nchini, ili kuhakikisha matokeo yake yanatumika ipasavyo katika maamuzi ya kisera na mipango ya maendeleo.
Amesisitiza kuwa tafiti hizo zitachangia maendeleo ya uchumi, jamii na mazingira, hasa katika kukabiliana na changamoto zinazoibuka ikiwemo ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa siku mbili unalenga kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za utafiti, ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Kwa ujumla, Tanzania inaendelea kujipanga kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, yakilenga kukuza uchumi shindani na jumuishi, kuongeza ajira na tija, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.
Akiwasilisha maada, Naibu Katibu Mtendaji – Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursali Milanzi amebainisha kuwa Tume ya Taifa ya Mipango ina jukumu la kusimamia na kushauri masuala ya uchumi, ikijumuisha kuchambua hali ya mfumuko wa bei, uwiano wa mapato na matumizi ya Serikali, pamoja na kuhakikisha uchumi unakuwa na utulivu na ukuaji endelevu. Pia ameongeza kuwa Tume inaratibu na kuongoza mipango ya kitaifa, kisekta na kitaasisi ili iendane na Dira ya Taifa na utekelezwe kupitia mipango ya muda mrefu, wa kati na wa mwaka.
Aidha, amesema kuwa Tume hufanya tathmini ya sera kuhakikisha zinatoa matokeo yanayotarajiwa na kutoa ushauri wa kuboresha pale inapobidi. Pia inahakikisha mipango ya sekta mbalimbali inafungamana na malengo ya kitaifa ili kuepuka migongano ya utekelezaji, huku ikiendelea kuimarisha taaluma ya mipango kupitia majukwaa kama Mkutano wa Wapangaji.