| Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiagana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, baada ya kikao kilichojadili masuala ya ushirikiano katika kukuza uchumi kati ya Tanzania na Austria, katika ukumbi wa mikutano wa Hazina, jijini Dar es Salaam. |
Na. Saidina Msangi na Josephine Majula, WF, Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Austria ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mkakati mpya wa Austria-Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 yanafikiwa kama yalivyopangwa.
Mhe. Munde alisema hayo alipokutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, katika kikao kilichojadili masuala ya mkakati wa Austria wa kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ikiwemo ushirikiano katika kukuza uchumi kati ya Austria na Tanzania, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa Mkakati huo mpya wa Austria-Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 umejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni amani na usalama, ushirikiano wa kiuchumi, uhamiaji, pamoja na elimu na sayansi.
‘‘Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iko tayari kushirikiana na Austria kutekeleza mkakati huo kwa maendeleo ya watu wa pande zote mbili na inatarajia kuona ushirikiano ukikua zaidi katika sekta za umma na binafsi,’’alieleza Mhe. Munde.
Alifafanua kuwa katika nyanja ya amani, pande zote mbili zinalenga kuimarisha uthabiti kupitia ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kuzuia migogoro, huku upande wa uchumi ukilenga kukuza uwekezaji na fursa za uchumi wa kijani ili kutengeneza ajira na kuboresha miundombinu.
Aidha, Mhe. Munde aliongeza kuwa mkakati huo utashughulikia suala la uhamiaji kwa kupambana na biashara haramu ya binadamu na kukuza uhamiaji wa kisheria wenye tija ambapo katika sekta ya elimu, kutaanzishwa vituo vya umahiri na programu za ufadhili wa masomo katika nyanja za maji, nishati, afya, na mifumo ya kidijitali.
Aliongeza kuwa Mkakati huu mpya unatazamwa kama daraja muhimu kuelekea Dira ya Tanzania 2050, ukisisitiza ushirikiano wa usawa na wenye faida kwa pande zote mbili na kutoa rai kwa sekta binafsi Austria kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana nchini ikiwemo katika sekta ya kilimo, nishati pamoja na mazingira ili kuweza kuwekeza nchini.
Pia Mhe. Munde aliishukuru Austria kwa msaada wake ambao unaendana na vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) pamoja na Dira ya Maendeleo ya 2025, wakati nchi ikielekea kuanza rasmi utekelezaji wa Dira mpya ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni.
‘’Austria inafadhili miradi mikubwa ya kimkakati nchini yenye thamani ya Euro milioni 30 kupitia mikopo nafuu katika ukarabati na uboreshaji wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Zanzibar kwa Euro milioni 7, uboreshaji wa mfumo wa elimu Zanzibar kwa Euro milioni 6, ununuzi wa magari ya zimamoto na vifaa vya uokoaji kwa upande wa Zanzibar kwa Euro milioni 10, pamoja na ukarabati wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) uliogharimu Euro milioni 7’’, alifafanua Mhe. Munde.
Kwa upande Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, alipongeza Tanzania kwa hatua inayoendelea nayo katika kukuza uchumi akieleza kuwa amani imechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia wawekezaji kutoka nje akisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kutumia fursa hiyo kujitangaza zaidi kuvutia wawekezaji.
Alisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kuhakikisha kuwa sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika fursa za uchumi ili kuweza kuziimarisha ziweze kuchangia katika kukuza ajira nchini na kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema nchi hiyo ina kampuni zinazofanya kazi nchini ikiwemo Andritz ambayo imechangia miradi ya umeme wa maji, mradi wa kahawa pamoja na mradi wa korosho ambapo uwepo wa kampuni za Austaria imechangiwa kwa kiasi kikubwa na amani iliyopo nchini hivyo kuna uwezekano wa nchi hiyo kuongeza uwekezaji zaidi.









