Featured Kitaifa

WAMILIKI WA LESENI ZA MADINI WAFUNDWA,TUME YASISITIZA UTEKELEZAJI WA SHERIA

Written by Alex Sonna

Dodoma

Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kusisitiza utekelezaji wa sheria na kanuni katika sekta ya madini, ikiwataka wamiliki wa leseni kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinawanufaisha watanzania na kulinda maslahi ya taifa.

Akizungumza jijini Dodoma kwenye kikao cha wamiliki wa leseni, Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, amesema kipaumbele cha Serikali ni kuwawezesha wamiliki wa leseni wazawa huku ikiweka msisitizo kwa wawekezaji wa kigeni kufuata taratibu zote za uwekezaji kabla ya kuanza shughuli zao.

Amesema ni lazima kwa mwekezaji wa kigeni kupata idhini kupitia Afisa Madini wa eneo husika kabla ya kuanza shughuli yoyote, sambamba na kuwa na utaalam maalum unaohitajika katika sekta hiyo.

“Ni wajibu wa mmiliki wa leseni kulinda utu na maslahi ya watanzania katika maeneo ya uchimbaji. Ni aibu kuona Mtanzania anadhulumiwa katika leseni inayomilikiwa na Mtanzania mwenyewe. Kanuni zipo, zifuateni,” amesema Mhandisi Mwasha.

Ameongeza kuwa wamiliki wa leseni wanapaswa kuzingatia masharti yote ya leseni zao, ikiwemo kuteua meneja mwenye uwezo wa kusimamia shughuli za uchimbaji na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi migodini.

Pia, Mhandisi Mwasha amekemea tabia ya baadhi ya wazawa kuwaingiza wawekezaji wa kigeni bila kufuata taratibu rasmi kupitia Ofisi za Madini, akisisitiza kuwa mikataba yote inapaswa kuwa halali na kusimamiwa na mamlaka husika.

“Wawekezaji wa kigeni wanapaswa kuheshimu mila na desturi za Watanzania, na pia kuhakikisha wana wataalam wanaoweza kuwasiliana kwa Kiswahili na Kiingereza. Serikali ipo kuwalinda na kuwatetea wazawa,” amesema.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Tume ya Madini, Hadija Ramadhan, amesema Tume inaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa leseni kuhusu kanuni za msaada wa kiufundi kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123.

Amefafanua kuwa wamiliki wa leseni ndogo za madini wanaruhusiwa kuingia mikataba ya msaada wa kiufundi na wawezeshaji lakini mikataba hiyo lazima iwe rasmi na kuthibitishwa na mamlaka za madini.

Ameongeza kuwa mwezeshaji anatakiwa kutoa msaada katika maeneo ya utafutaji, uchimbaji, matumizi ya mitambo na teknolojia pamoja na uchenjuaji, huku vifaa vyote vikiorodheshwa kwenye mkataba na kubaki kwa mmiliki wa leseni endapo mkataba utasitishwa.

Kwa upande mwingine, Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Theresia Numbi amesisitiza umuhimu wa wamiliki wa leseni kuelewa mikataba kabla ya kuingia ubia, akiwahimiza kutumia wataalam wa sheria.

“Mkataba ni nyenzo muhimu sana. Tafuta mwanasheria akusaidie kuutafsiri kabla ya kusaini. Ni bora kulipa gharama ndogo sasa kuliko kupata hasara baadaye,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wadau wa sekta ya madini kufanya vikao vya tathmini mara kwa mara ili kufuatilia mapato, changamoto na mafanikio ya shughuli zao.

About the author

Alex Sonna