Njombe
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Kilomita 8.3 katika Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Samson Medda ambapo amefafanua kuwa mradi huo utaogharimu takribani Shilingi Bilioni 20 upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi wa ofisi ya mradi yenye gorofa moja, ujenzi wa mifereji pamoja na taa za barabarani.
”Mradi huu utasaidia katika kuboresha barabara zetu ambapo barabara tano (5) zitajengwa kwa kiwango cha lami zikiwemo NBC-Kibena Km 2.85, Mpechi-Melinze Km 1.3,
Chaugingi-Zwengelendete Km 1.5,
Zwengelendete-Masaki Km 1.4 na Magereza-Matalawe Km 1.1″, amesema.
Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo kutoka TARURA, Mhandisi Deo Octavian amesema kuwa mradi huo tayari upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kwamba kwa upande wa jengo la usimamizi wa mradi tayari kazi inaendelea na kwa upande wa barabara nako kazi inaendelea.
”Mkandarasi ameanza kazi katika Jengo la usimamizi wa mradi na katika barabara kazi pia inaendelea, kukamilika kwa barabara hizi kutarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi lakini pia mji utapendeza hasa ukizingatia kwamba barabara hizi zitawekewa taa”, amesema.
Bw. Niko Vitus ambaye ni mkazi wa Njombe ameipongeza Serikali kwa ujio wa mradi huo kwani kipindi cha masika barabara hupitika kwa shida na hivyo huwachukua muda mrefu kutoka eneo moja hadi lingine na kuzorotesha shughuli za kiuchumi.
”Tunaipongeza Serikali kwa kuiona changamoto hii ambapo kukamilika kwa barabara hizi itasaidia kusafiri kwa urahisi katika kuyafikia maeneo mbalimbali”, amesema.
Naye, Bw. Alex Mwalongo mkazi wa Njombe amesema kuwa licha ya mji wa Njombe kupendeza baada ya kukamilika kwa mradi huo pia shughuli za kiuchumi zitakuwa kwa wananchi.
Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa mji wa Njombe utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwaka 2027.
