Na.Alex Sonna-Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni tano kufadhili wanafunzi wanaochaguliwa kusoma masuala ya Akili Unde, Sayansi na Teknolojia katika ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamili, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuijengea nchi wataalamu wanaoendana na mabadiliko ya dunia ya sasa ya kidijitali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 25,2026 Mtumba jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, amesema mpango huo umeanza kutekelezwa kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi 10 wa Shahada ya Uzamili wanaosoma katika Nelson Mandela African Institution of Science and Technology katika fani za Akili Unde na Sayansi na Teknolojia.
Aidha Prof.Mkenda amesema kuwa wanafunzi wengine 10 wanatarajiwa kupelekwa kusoma katika Indian Institute of Technology Madras Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kuimarisha uwezo wa kitaifa katika taaluma za kimkakati.
“Akili Unde itafanya mambo mengi katika sekta mbalimbali. Kama nchi, lazima tujijengee uwezo kwa kuwa na wataalamu wa kutosha. Rais ameliona hili na ndiyo maana amesisitiza vijana wetu wapate fursa hizi,” amesema Prof. Mkenda.
Amesema Serikali tayari imeanza kutekeleza ahadi ya Rais ya kupeleka vijana kusoma Sayansi ya Data, Akili Unde na taaluma nyingine muhimu nje ya nchi kupitia mpango wa Samia Scholarship.
Hata hivyo amesema kuwa wanafunzi 16 tayari wamepelekwa kusoma nchini Afrika Kusini, huku wengine 34 wakitarajiwa kwenda Ireland mwezi Julai mwaka huu.
Amesisitiza kuwa uwekezaji huo katika elimu ya juu ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuingia katika uchumi wa maarifa, unaotegemea zaidi ubunifu, teknolojia na ujuzi wa hali ya juu.
Aidha, wanafunzi waliopata ufadhili kupitia Samia Scholarship katika ngazi ya Shahada ya Kwanza wametakiwa kuangalia majina yao kupitia tovuti ya Wizara (www.moe.go.tz), Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (www.costech.or.tz) na tovuti ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Prof.Amos Nungu, amesema taasisi hiyo inajivunia kuratibu programu hiyo ambayo imepokelewa kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa wanafunzi na vyuo vya kimataifa.
Ameeleza kuwa vyuo mbalimbali nje ya nchi tayari vimeanza kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kupokea wanafunzi kupitia mpango huo.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof.Maulilio Kipanyula, amesema taasisi hiyo haikuchaguliwa kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na hadhi yake ya kimataifa. Amebainisha kuwa takribani asilimia 10 ya wanafunzi wake wanatoka nje ya nchi, hali inayowawezesha wanafunzi kupata mazingira ya kimataifa mapema.
Profesa Kipanyula ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika taasisi hiyo ni wahadhiri wa vyuo vikuu, hivyo uwekezaji unaofanywa kupitia Samia Scholarship Extended unachangia kujenga msingi imara wa wataalamu wa ndani.
Amesema taasisi hiyo tayari imezalisha zaidi ya wahadhiri 350 wa vyuo vikuu nchini na itaendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya elimu ya juu ya sayansi na teknolojia.




