Featured Kitaifa

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA MSAADA WA KISHERIA NA HAKI

Written by Alex Sonna

 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, leo Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam amefungua Kongamano la Nchi za Afrika Mashariki kuhusu mchango wa teknolojia katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki (The East Africa Legal Tech for Legal Aid and Access to Justice Symposium – 2026).

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Katimba amesema kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua za makusudi katika kuimarisha upatikanaji wa haki chini ya Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017.

“Tunaendelea kupanua huduma za msaada wa kisheria kwa kushirikiana kwa karibu na mashirika ya kiraia pamoja na mitandao ya wasaidizi wa kisheria (paralegals) ili kufikia jamii ambazo hazijahudumiwa ipasavyo,” amesema Mhe. Katimba.

Aidha, ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania imeboresha mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa mashauri, usikilizwaji wa kesi kwa njia ya mtandao, pamoja na uwekaji wa kumbukumbu za mahakama katika mfumo wa kidijitali hatua ambazo zimeongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa wananchi.

Kongamano hilo la siku mbili linatarajiwa kujadili na kubainisha namna ambavyo teknolojia inaweza kutumika kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma za msaada wa kisheria na kuimarisha upatikanaji wa haki Afrika Mashariki.

About the author

Alex Sonna