Featured Kitaifa

WAZIRI WA ULINZI NA JKT AFANYA ZIARA KUKAGUA MRADI WA UJENZI WA UWANJA WA KIMATAIFA WA GOLF

Written by Alex Sonna
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt Rhimo Nyansaho (Mb) tarehe 20 Februari, 2026, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwanja mkubwa kimataifa wa mchezo wa Golf unaojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika eneo la Ihumwa, jijini Dodoma.
Mradi huu wa kimkakati unaojumuisha viwanja 18 vya mchezo huo, hoteli kubwa ya kisasa ya hadhi ya Nyota Tano, na miundombinu ya michezo mbalimbali umejumuisha mabwawa ya kuogelea na bustani ya wanyama (ZOO) ambapo hadi sasa jumla ya viwanja tisa tayari vimekamilika,hii ikiwa ni kudhihirisha weledi na kasi ya kipekee ya JWTZ katika kutekeleza miradi ya Kimkakati ya maendeleo kwa ufanisi wa hali ya juu na kuchangia pato la Taifa kupitia Diplomasia ya michezo.
Uwanja wa Kimataifa wa Mchezo wa Golf wa Ihumwa mara tuu utakapokamilika unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vikubwa na vya kisasa zaidi kuwahi kujengwa hapa nchini, ukifuatiwa kwa ukubwa na uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club uliopo jijini Dar es Salaam, ambao pia unamilikiwa na kuendeshwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Uwepo wa uwanja huu katika Makao Makuu ya nchi,Dodoma utaweka rekodi mpya katika tasnia ya michezo na utalii nchini na kuchangia maendeleo ya Kiuchumi kwa Taifa huku ukiongeza hadhi ya Tanzania katika medani za kimataifa za mchezo wa Golf. 
Waziri wa Ulinzi Dkt Rhimo Nyansaho amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huu kutaifanya Dodoma kuwa kitovu cha michezo ya kitalii na mikutano mikubwa ya kimataifa kutokana na ubora wa miundombinu inayojengwa.
Mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji, Dkt Rhimo Nyansaho amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutekeleza kwa ufanisi maono ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,akaongeza kwa kusema kuwa Mheshimiwa Rais Samia aliridhia kwa JWTZ kujenga mradi huo wa kisasa ili kuongeza thamani ya ardhi ya Ihumwa na kutoa huduma bora za hadhi ya kimataifa. 
Waziri wa Ulinzi na JKT amesema kuwa, uwekezaji huu ni kielelezo cha namna Jeshi linavyoweza kutumia rasilimali zake kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya michezo na ukarimu.
Dkt Rhimo Nyansaho akahitimisha ziara yake kuwapongeza viongozi wa JWTZ kwa kuwa na maono ya kuasisi na kuanza kutekeleza mradi huu kabambe ambao utakuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa jeshi na nchi, huku ukitumika kuitangaza Tanzania duniani kote. 
Waziri Rhimo Nyansaho akatoa pongezi pia kwa Kamati ya Ujenzi ya uwanja huo kwa uratibu mzuri na weledi uliowezesha mradi kufikia hatua kubwa ndani ya muda mfupi. Waziri wa Ulinzi na JKT akatoa wito kwa kamati hiyo kuendelea na kasi hiyo ili mradi uweze kukamilika kwa wakati ili uanze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa manufaa ya Taifa. 

About the author

Alex Sonna