Wakulima wa zao la pamba mkoa wa Simiyu ambao ni wanachama wa Vyama vya Ushirika wameshauriwa kulima kwa tija kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuepukana kilimo cha mazoea ambacho kinawapa hasara.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha katika Mkutano wa 8 Chama Kikuu Simiyu, SIMCU (2018) LTD, uliofanyika leo Februari 20, 2026 Wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu, pia amewaahakikishia wakulima kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha kwa kutoa rudhuku za mbolea, viuatilifu na kutafuta masoko ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
“Mkulima anapata kilo mia tatu za pamba kwa heka ni hasara na ni upotevu wa muda inabidi tutoke kwenye kilimo cha namna hii…” alisema Mhe. Macha
Akizungumza kwa niaba ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Consolata Kiluma, ambaye ni Naibu Mrajis – Uhamasishaji, amewasistiza wajumbe wa bodi za vyama vya Ushirika kuwa waadilifu na waaminifu katika kutekeleza majukumu, na kuwa wabunifu kuleta ushindani kwenye biashara kama kauli mbiu isemavyo “Ushirika ni Biashara” ili kuongeza mapato kwa maslahi ya wanaushirika na Wananchi kwa ujumla.
Aidha, Mrajis Msaidizi Mkoa wa Simiyu Godfrey Mpepo amesema Ushirika umeendelea kuimarika tangu kilipoanzishwa chama kikuu SIMCU Ltd mwaka 2018, ambapo awali vyama vya mkoa huo vilikuwa vikisimamiwa na SHIRECU chama kikuu kutoka mkoa wa Shinyanga.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsha Mohamed amewataka wajumbe wa Mkutano huo kuepuka na ubadhilifu wa fedha za wanachama jambo ambalo linarudisha Ushirika nyuma kimaendeleo.
Awali, akitoa taarifa ya Utendaji wa SIMCU(2018) LTD, Meneja Mkuu wa chama hicho, Mercy Atanazi alibainisha kuwa mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 625 kati ya wajumbe 675 kutoka vyama wanachama 335.



