Featured Kimataifa

DC BAGAMOYO APONGEZA JUHUDI ZA TANESCO KATIKA KUHAMASISHA MATUMIZI NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Written by Alex Sonna

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mheshimiwa Shaibu Ndemanga, amepongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kulinda afya za wananchi na mazingira.

Mheshimiwa Ndemanga alitoa pongezi hizo wakati akipokea jiko la umeme linalotumia nishati kidogo, lililotolewa na TANESCO, alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania (SHISAMA), uliofanyika katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA) tarehe 17 Februari, 2026.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa jiko hilo, Mheshimiwa Ndemanga alisema kuwa matumizi ya nishati safi ya umeme ni sehemu ya utekelezaji wa mwelekeo wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanatumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.

“Naipongeza TANESCO kwa kuendelea kuelimisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi ya umeme ambayo inalinda afya za wananchi na mazingira yetu,” alisema Mhe. Ndemanga.

Aidha, aliiomba TANESCO kushirikiana na wasanii wa SHISAMA kwa kuwatumia kama mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia sanaa zao.

“Wasanii wana nafasi kubwa ya kuifikia jamii. Wakishirikishwa kikamilifu, wanaweza kusaidia kueneza elimu ya nishati safi kwa ufanisi zaidi,” aliongeza.

Kwa upande wa TANESCO, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Mkoa wa Pwani Kaskazini, Bi. Esther Msaki, alisema kuwa utoaji wa majiko ya umeme ni sehemu ya mkakati wa TANESCO wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kwa matumizi ya majumbani.

“TANESCO inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maana ya nishati safi, umuhimu wake pamoja na faida zake, ikiwemo kupunguza gharama za nishati, kulinda afya na mazingira,” alisema Bi. Msaki.

Katika tukio hilo, TANESCO pia iliwapatia majiko ya umeme viongozi wa SHISAMA akiwemo Rais wa Shirikisho hilo, Makamu wa Rais pamoja na Mwenyekiti, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia sanaa zao.

About the author

Alex Sonna