Featured Kitaifa

HEMED: ULINZI NA USALAMA NI MSINGI WA HAKI NA MAENDELEO

Written by Alex Sonna

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema msingi mkubwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kuhakikisha inalinda wananchi na mali zao pamoja na kutenda haki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi uliofika ofisini kwake Baraza la Wawakilishi, Chukwani Zanzibar, kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema suala la usalama wa raia na mali zao ni jambo muhimu katika kuimarisha shughuli mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ameeleza kuwa kwa kuzingatia umuhimu huo, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu nchini wakati wote.

Mhe. Hemed amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria na miongozo mbalimbali ili kuimarisha utawala bora katika kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutumia teknolojia katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Sambamba na hayo, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano na miongozo stahiki ili kuhakikisha wanatekeleza maagizo yote yanayotolewa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa yale yote aliyokusudia kuyatimiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Pascal Katambi (Mb), amesema dhamana waliyopewa ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao ni kubwa. Hata hivyo, ameahidi kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kwa kufuata misingi ya kikatiba, kisheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali.

Waziri Katambi amesema watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi watafanya kazi kwa bidii na nidhamu kwa kuhakikisha wanalinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuulinda Muungano wake na kulinda tunu za Taifa ili kuendelea kuiletea heshima Tanzania ndani na nje ya mipaka yake.

Amewapongeza viongozi wakuu wa nchi kwa kuliongoza Taifa kwa kufuata misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu na ustawi wa wananchi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Katika ziara hiyo, Mhe. Katambi ameambatana na Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; Ndugu Ally Senga Gugu, Katibu Mkuu; pamoja na Ndugu Miriyam Pereele Mmbanga, Mkurugenzi wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.  

About the author

Alex Sonna