Featured Kitaifa

CCM YAENDELEA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO MKOA WA MWANZA

Written by Alex Sonna

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu John Mongella, ameeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Mwanza, akihitimisha maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM.

Akizungumza mbele ya Wanachama wa CCM na Wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Mongella amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za elimu, maji, afya na miundombinu ili kuboresha maisha ya Wananchi.

Katika sekta ya maji, amesema Serikali inatekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi maeneo ya vijijini na mijini, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 264.8 zimetumika katika miradi ya maji vijijini, shilingi bilioni 164.4 kwa miradi ya maji mijini, pamoja na shilingi bilioni 196.8 katika utekelezaji wa miradi ya elimu inayohusiana na miundombinu.

Ameongeza kuwa mradi wa maji kutoka Ukiringo – Koromije – Sumve unaendelea kutekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 32, huku hatua za mwisho za mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Sumve zikiendelea ili kuhakikisha Wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika.

Katika sekta ya Afya, Ndugu Mongella amesema Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 900 katika ujenzi na uboreshaji wa vituo vya Afya, Hospitali na ununuzi wa vifaa tiba mkoani Mwanza, hatua iliyosaidia kusogeza huduma za afya karibu zaidi na Wananchi.

Aidha, amesema katika sekta ya vivuko, Serikali imetenga shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kuboresha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria, hatua inayolenga kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Ndugu Mongella amewahimiza Wananchi wa Mwanza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kusimamia miradi hiyo ili iwe na tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo, huku akisisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani yake kwa vitendo.

Mwisho, ametoa wito kwa Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla kuendelea kukiamini Chama hicho na kuimarisha mshikamano, akisema mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya CCM ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.

About the author

Alex Sonna