Featured Kitaifa

SIKU 100 ZA RAIS:SERIKALI YATENGA BILIONI  5 KUWEZESHA KAMPUNI CHANGA 50 ZA TEKNOLOJIA

Written by Alex Sonna

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 4,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kipindi cha Uongozi wake katika awamu ya sita.

Na.Alex Sonna-Dodoma

Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuziwezesha Kampuni Changa (Startups) 50 kupitia mikopo yenye riba nafuu itakayokuwa ikitolewa na benki za biashara, lengo likiwa ni kukuza bunifu za teknolojia na kuongeza ajira kwa vijana.

Hayo yamesemwa leo Februari 4, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 za uongozi wa Rais katika muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Mhe. Kairuki amesema fedha hizo zitaelekezwa kusaidia bunifu zinazojikita katika sekta mbalimbali ikiwemo Fedha (FinTech), Afya, Kilimo, Elimu, Utalii, Akili Unde (AI), Bima, Usafirishaji, Lishe pamoja na Teknolojia za Sheria. Alifafanua kuwa kila Kampuni Changa inatarajiwa kuajiri watu kati ya saba hadi 10, hivyo kuchangia moja kwa moja katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

 “Wizara imeanza taratibu za kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups Development Fund) ili kuhakikisha upatikanaji wa mitaji endelevu kwa wabunifu, ambao mara nyingi hukosa dhamana zinazohitajika na taasisi za kifedha.”amesema Mhe.Kairuki

Aidha  Mhe. Kairuki amesema kuwa Wizara imekamilisha rasimu ya Sera ya Kampuni Changa ya Mwaka 2026 ambayo kwa sasa ipo katika hatua za uidhinishwaji Serikalini.

Amesema sera hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kukuza bunifu, kuongeza ajira na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya TEHAMA.

Pia, Kampuni Changa 158 zimeshatambuliwa na kusajiliwa kupitia mfumo wa SAFARI HUNT, huku Serikali ikikamilisha maandalizi ya kuwawezesha kushiriki katika zabuni za umma kupitia Mfumo wa Manunuzi ya Umma (NEST).

Waziri amesema kuwa  Serikali imeanza taratibu za ujenzi wa Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Kidijitali (NDTI) jijini Dodoma kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 167.3.

Amesema chuo hicho kitalenga kutoa mafunzo ya vitendo katika teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Unde (AI), Usalama wa Mtandao, Uchambuzi wa Data, Roboti na Mtandao wa Vitu (IoT).

Wakati ujenzi ukiendelea, Serikali imeanzisha ushirikiano na vyuo vikuu vya UDSM, UDOM, SUZA na MUST kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.9 ili kuanza kutoa mafunzo hayo mapema.

Katika kuimarisha uwajibikaji, Mhe. Kairuki amesema taasisi 800 za umma zimeunganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali (GovNet), hatua iliyosaidia wananchi kuwasilisha kero na kupata majibu kwa njia ya kidijitali.

Ameongeza kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za majaribio ya Mfumo wa Tembo Portal, ambao utawawezesha wananchi kuweka miadi ya kukutana na viongozi wa Wizara kidijitali, huku uzinduzi wake ukitarajiwa kufanyika Aprili 2026.

Kwa upande wa mawasiliano, Waziri amesema kuwa  idadi ya laini za simu imeongezeka kutoka milioni 99.3 Oktoba 2025 hadi milioni 106.9 Januari 2026. Watumiaji wa intaneti wamefikia milioni 58.1, huku watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu wakifikia milioni 76.5.

“Gharama za mawasiliano zimeendelea kuwa nafuu, ambapo gharama ya kupiga simu ndani ya nchi imebaki Shilingi 29 kwa dakika na bei ya data bila kifurushi ikiwa Shilingi 9.35 kwa MB.”ameongeza

Katika kipindi cha siku 100, Wizara imekamilisha ujenzi wa minara 758 katika kata 713 nchini, huku ujenzi wa minara mingine 636 vijijini ukiendelea na kufikia utekelezaji wa asilimia 78.

Aidha, Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa minara 201 katika maeneo ya barabara kuu, reli, mipakani na hifadhi za taifa. Kwa upande wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, wilaya 119 kati ya 139 zimeunganishwa, sawa na asilimia 86, huku wilaya 20 zilizobaki zikitarajiwa kuunganishwa ifikapo Juni 2026. Huduma ya Wi-Fi ya umma imefikishwa katika maeneo 61 nchini.

Mhe. Kairuki amesema kuwa  Wizara imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 132, sawa na asilimia 109.9 ya lengo, hali iliyochangiwa na matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeanza utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na satelaiti yake, ambapo taratibu za utungaji wa Sera na Sheria ya Anga za Juu zimeanza, sambamba na maandalizi ya uundaji wa satelaiti kwa kushirikiana na vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo Mhe. Kairuki amesema kuwa utekelezaji wa ahadi za siku 100 umeweka msingi imara wa kujenga uchumi wa kidijitali unaojumuisha wananchi wote, huku akiwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuiamini Serikali ya Awamu ya Sita.

About the author

Alex Sonna