Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI MAKAMBA AZINDUA MRADI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA SHULE YA SEKONDARI BUNGE WASICHANA

Written by Alex Sonna

Na.Alex Sonna-Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba,amezindua  rasmi Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana iliyopo jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kulinda afya, mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika taasisi za umma.

Akizindua mradi huo  Mhe. Makamba kwa niaba ya  Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratias Ndejembi,amesema   mradi huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

 Mhe. Makamba,ameeleza  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ndani na nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia.

 “Matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025, ingawa bado asilimia 77 ya kaya hutumia nishati isiyo safi, hali inayosababisha vifo vya takribani watu 33,000 kila mwaka kutokana na magonjwa yatokanayo na moshi wa majumbani pamoja na uharibifu wa mazingira.”amesema Mhe.Makamba

Mhe. Makamba amebainisha kuwa shule ya Sekondari Bunge Wasichana imechaguliwa makusudi kwa kuwa ni miongoni mwa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, huku Serikali ikiwa tayari imetoa katazo kwa taasisi hizo kuacha matumizi ya kuni na mkaa.

Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo mpya, chakula kitapikwa kwa haraka, usafi na ufanisi mkubwa bila kuathiri afya za wapishi na wanafunzi.

Aidha, amesema kuwa hadi sasa zaidi ya taasisi 1,136 nchini zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, jambo alilolitaja kuwa ni la kujivunia, huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Makamba amezindua Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia ya Shule ya Sekondari Bunge Wasichana (Clean Cooking School Club), klabu ya kwanza ya aina yake nchini.

Amesema kuwa klabu hiyo itakuwa na jukwaa la kuwaandaa wanafunzi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia mashuleni na katika jamii zinazowazunguka.

Hata hivyo amesisitiza kuwa utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia unahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo sekta binafsi, taasisi za kifedha, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

Amewahimiza wafanyabiashara, wabunifu na vijana vyuoni kubuni teknolojia rafiki zitakazowezesha upatikanaji na matumizi ya nishati safi, hususan maeneo ya vijijini na pembezoni.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Naibu Katibu Mkuu Nishati, James Mataragio, amesema tafiti zinaonesha zaidi ya watu milioni mbili hufariki kila mwaka duniani kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia, huku nchini Tanzania athari hizo kubwa zaidi zikiwa kwa wanawake na watoto.

Amesema uzinduzi wa mradi huo ni utekelezaji wa sera ya taifa inayolenga kuondokana na matumizi ya nishati isiyo salama na kujikita katika matumizi ya nishati safi, hatua itakayosaidia kulinda mazingira, kuboresha afya na kuongeza tija hata katika ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweru, amesema Shule ya Sekondari Bunge Wasichana ni miongoni mwa shule vinara wilayani humo na kuipongeza Serikali kwa kuifanya shule hiyo kuwa kipaumbele cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Mhe. Jonas Mbunda, amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wote, huku Kamati ikiridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati nchini.

 Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bunge Wasichana, Richard Msana alisema shule hiyo yenye wanafunzi 555 imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati ya kupikia baada ya kuachana na matumizi ya kuni na kuhamia katika gesi.

Amesema kuanzia Julai 2020 hadi Mei 2022, shule ilikuwa ikitumia takribani shilingi milioni 10.5 kwa kila miezi mitatu kununua kuni. Baadaye walipoanza kutumia mkaa mbadala, gharama zilishuka hadi kufikia shilingi milioni 2.7 na hivi sasa, kupitia mradi wa matumizi ya gesi, shule imenunua tani moja ya gesi iliyotumika kwa miezi miwili, ambapo matumizi ni wastani wa shilingi milioni 1.3 kwa mwezi, kiwango ambacho ni nafuu zaidi kiuchumi.




About the author

Alex Sonna