Featured Kitaifa

SIKU 100 ZA RAIS SAMIA:VIFAA VYA KIDIGITALI VYASAMBAZWA KWA WALIMU WENYE ULEMAVU NCHINI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 31,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kipindi cha Uongozi wake katika awamu ya sita.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI  wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha elimu jumuishi na mafunzo ya ujuzi kwa vitendo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 za muhula wa pili.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Januari 31,2026 kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan, Prof. Mkenda amesema kuwa Wizara imenunua na kusambaza vifaa vya kidijitali na saidizi vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.35 kwa walimu na walimu tarajali wenye ulemavu katika halmashauri zote 184 nchini, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wote bila ubaguzi.

“Hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kutekeleza elimu jumuishi kwa vitendo, kwa kuhakikisha walimu wenye ulemavu wanapata vifaa stahiki vinavyowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” amesema  Prof. Mkenda.

Aidha, Waziri amesema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo 64 vya Ufundi Stadi (VETA) ngazi ya wilaya, ambapo ujenzi wake umefikia wastani wa asilimia 67.

 “Vyuo hivyo vikikamilika vitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi takribani 33,000 kwa mwaka katika fani mbalimbali za ujuzi, jambo litakaloongeza fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana.”amefafanua Prof. Mkenda.

 Prof.Mkenda amesema  kuwa miongoni mwa ahadi kuu za Rais Samia ni kuimarisha elimu ya msingi, hususan umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa elimu ya awali hadi darasa la tatu.

Amesema Wizara imeandaa na kukamilisha Mkakati wa Kisayansi wa Miaka Mitano wa Kujenga Umahiri wa KKK, unaobeba kauli mbiu “Elimu ya Awali Msingi wa Maendeleo Endelevu”, ambao umezinduliwa rasmi na Rais Samia tarehe 29 Januari, 2026.

“Lengo letu ni kuhakikisha kila mtoto anapofikia darasa la tatu awe na umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu bila shida. Hatuna sababu katika karne hii kuwa na changamoto ya KKK,” amesema Prof. Mkenda.

Hata hivyo  ameongeza kuwa utekelezaji wa mkakati huo umevutia wadau wa maendeleo, akitaja UNICEF ambao wameahidi kuchangia shilingi bilioni 2 kwa ajili ya mafunzo ya walimu.

 Amesema Serikali imeajiri walimu 6,044 kati ya walimu 7,000 wa masomo ya sayansi na hisabati waliopangwa kuajiriwa, huku taratibu za ajira kwa walimu waliobaki zikiendelea kukamilishwa.

Kuhusu mafunzo ya ujuzi na ajira kwa vitendo, Prof. Mkenda amesema Wizara kwa kushirikiana na waajiri, vyuo vya ufundi stadi (VETA) na vyuo vikuu imeandaa Mfumo wa Pamoja (Framework) wa kulinganisha mafunzo na mahitaji ya soko la ajira katika sekta za kipaumbele ikiwemo nishati, TEHAMA na viwanda, ambao unatarajiwa kuzinduliwa Februari 9, 2026.

“Tunapanga pamoja na tunatekeleza pamoja. Kiunzi hiki kitaondoa pengo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira,” amesisitiza.

Aidha Waziri Mkenda amesema Serikali imeongeza kwa kiasi kikubwa mikopo ya elimu ya juu, ambapo ndani ya mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya wanafunzi 276,032 wamenufaika na mikopo kupitia HESLB yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 899.

Aidha, kupitia Samia Scholarship, Serikali imetoa ufadhili kwa wanufaika 3,137 ndani na nje ya nchi katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati, tiba na TEHAMA, ikiwa ni pamoja na sayansi ya data na akili unde (AI).

Serikali pia imekamilisha ujenzi wa shule 26 maalum za sayansi kwa wasichana na shule 5 za vipaji kwa wavulana, huku nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

 Prof. Mkenda amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa kampasi mpya za vyuo vikuu katika mikoa 15, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa majengo na uwekaji wa mawe ya msingi katika mikoa ya Kagera, Lindi na Zanzibar.

Prof. Mkenda amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 yanaonesha wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

About the author

Alex Sonna