Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. Ridhiwani Kikwete,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 30,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kipindi cha Uongozi wake katika awamu ya sita.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. Ridhiwani Kikwete,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 30,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kipindi cha Uongozi wake katika awamu ya sita.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete,amesema hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya vituo vya kazi kwa watumishi wapya wa ajira katika sekta ya umma, akibainisha kuwa nafasi hizo zimetolewa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila Halmashauri au mwajiri husika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 30,2026 kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,Mhe.Kikwete ,amesema kuwa kubadili kituo cha kazi kunaweza kuathiri idadi ya watumishi waliopangwa kwa kila Halmashauri, jambo ambalo lingesababisha ugawaji wa ajira kushindikana kufanyika kwa usahihi.
“Hivyo, kubadili kituo maana yake ni kupunguza idadi ya watumishi waliopangwa kwenda Halmashauri husika. Ili kutoathiri ugawaji wa nafasi hizi, hakuna mabadiliko yoyote ya vituo yatakayofanyika,”amesema Mhe.Kikwete
Aidha amesisitiza umuhimu wa kufuata mpangilio uliowekwa kwa uangalifu ili kuhakikisha ajira zinatekelezwa kwa usahihi.
Hata hivyo Mhe. Kikwete, amewaonya waajiriwa wapya katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 tangu kupokea barua za kupangiwa, akisisitiza kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watapoteza nafasi zao.
Kikwete amesema nafasi zitakazoachwa na waajiriwa watakaokiuka masharti hayo zitachukuliwa na wasailiwa wengine waliopo kwenye kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
“Natoa maelekezo kwa waajiri kuhakikisha kuwa baada ya kuwapokea watumishi wa ajira mpya, wanawasilisha taarifa zao za ajira kwa Mhariri Mkuu wa Gazeti la Serikali, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili ziweze kuchapishwa rasmi katika Gazeti la Serikali.”amesisitiza
Amesema jumla ya watumishi wa ajira mpya 8,416 kati ya 12,000 zilizoahidiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari wamepangiwa vituo vya kazi na kuripoti kazini.
Amefafanua kuwa miongoni mwa watumishi hao, baadhi tayari wameanza kulipwa mishahara yao kwa kuzingatia maelekezo ya Rais kwamba watumishi wapya watakaoripoti kazini kabla ya mwisho wa Januari waingizwe moja kwa moja kwenye mfumo wa mishahara.
Alikumbusha kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Rais Samia alitoa ahadi ya kutoa ajira mpya 12,000 katika sekta za elimu na afya, ahadi iliyopangwa kutekelezwa ndani ya siku 100 za mwanzo wa utawala wake.
“Baada ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuapishwa Novemba 3, 2025, kibali cha ajira ya watumishi 12,000 kilitolewa. Kwa mujibu wa kifungu cha 32(7) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, jukumu la kuendesha mchakato wa ajira linafanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, hivyo Sekretarieti ilitangaza nafasi hizo,” amesema Kikwete.
Aidha ameeleza kuwa baada ya kupokea maombi, Sekretarieti ya Ajira (PSRS) iliratibu mchakato wa usaili uliofanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na vituo maalum vya Unguja na Pemba. Usaili wa mchujo (aptitude test) ulifanyika kwa njia ya kidijitali Desemba 13 na 14, 2025, na matokeo kutolewa siku hiyo hiyo.
“Tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2025 ulifanyika usaili wa mahojiano kwa waombaji wote waliofaulu usaili wa mchujo,” amesema
Ameongeza kuwa kuanzia Januari 11 hadi 20, 2026, Sekretarieti ya Ajira iliwapanga vituo vya kazi waombaji wote waliofaulu, huku barua za kupangiwa vituo zikitumwa moja kwa moja kwenye akaunti za waombaji badala ya kufuatwa makao makuu ya Sekretarieti jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi sasa watumishi 8,416 wameripoti katika halmashauri mbalimbali nchini, wakiwemo 3,694 wa kada ya elimu na 4,722 wa kada ya afya. Kati yao, watumishi 735 walioripoti kabla ya kufungwa kwa orodha ya mishahara tayari wameingizwa kwenye mfumo wa mishahara ya Serikali na kulipwa mshahara wa Januari 2026.
Amesema watumishi wengine 956 wa elimu na 305 wa afya wapo kwenye mchakato wa kuingizwa kwenye mfumo huo, huku akisisitiza kuwa watumishi wote wataendelea kuingizwa kwenye payroll kadri wanavyoripoti kazini.