Featured Kitaifa

WAZIRI MAVUNDE ATOA TAARIFA YA MAFANIKIO MAKUBWA YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

Written by mzalendo

Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za kipindi cha Uongozi wake katika awamu ya sita.

Na.Alex Sonna – DODOMA

Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa ahadi na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 za kipindi cha pili cha uongozi wake katika Awamu ya Sita, hatua inayoendelea kuipa Sekta ya Madini mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Akizungumza leo Januari 26,2026 na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mhe.Mavunde,amesema kuwa taarifa hiyo imejikita katika maeneo 10 ya kimkakati yanayochochea ukuaji wa sekta na kuimarisha ustawi wa wananchi wanaofaidika na rasilimali za madini.

Makusanyo Ya Maduhuli Yapaa Kwa Kiwango Cha Rekodi
Waziri Mavunde,amefafanua kuwa makusanyo ya sekta hiyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 213.36 mwaka 2016/17 hadi kufikia Sh trilioni 1.07 mwaka 2024/25, sawa na asilimia 107.13 ya lengo lililowekwa. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 pekee, sekta imekusanya Sh bilioni 653.94, ambazo ni asilimia 108.99 ya lengo kwa kipindi hicho.

“Kati ya Novemba 2025 na Januari 25, 2026, jumla ya Sh bilioni 311.80 zimekusanywa, sawa na asilimia 111 ya lengo la Sh bilioni 280.64. Amesema mafanikio hayo yametokana na uimarishaji wa mifumo ya usimamizi, udhibiti wa biashara ya madini na mapambano dhidi ya utoroshaji wa madini.”amesema Mhe.Mavunde

Sekta Ya Madini Yapanda Katika Pato La Taifa
Amesema Sekta ya Madini imeendelea kukua kwa kasi ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 mchango huo ulifikia asilimia 11 na kuongezeka hadi asilimia 12 katika robo ya pili.

Uongezaji Thamani Wa Madini Waongezeka
Waziri Mavunde amesema kuwa maandalizi ya Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini wa miaka mitano (2026/27 – 2030/31) yamefikia hatua nzuri, huku viwanda vya uongezaji thamani vikipangwa kujengwa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Kahama, Mbeya, Lindi na Pwani.

Aidha, amesema ujenzi wa jengo la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) unaendelea, mradi ukiwa umefikia asilimia 10. Tani 14.66 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 3.75 zimeuzwa katika viwanda vya usafishaji dhahabu nchini kati ya Julai na Desemba 2025, huku BOT ikiongeza akiba ya dhahabu kwa kununua tani 17.03 zenye thamani ya Sh trilioni 4.97.

“Wizara kupitia STAMICO pia iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mtambo wa kusafisha chumvi uliopo Kilwa, wenye uwezo wa kuzalisha tani 24,480 kwa mwaka, unaotarajiwa kuanza kazi Februari 2026.”amesema

Ajira Kwa Watanzania Zaongezeka Kwa Kasi
Akizungumzia ushiriki wa Watanzania katika miradi ya madini (local content), Waziri Mavunde amesema kuwa ajira zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi 18,853 mwaka 2024, sawa na asilimia 97 ya ajira zote katika sekta hiyo mwaka huo.

Manunuzi ya bidhaa na huduma kwa kampuni za Kitanzania yaliongezeka kutoka Sh trilioni 1.85 mwaka 2018 hadi Sh trilioni 4.41 mwaka 2024, sawa na asilimia 88 ya manunuzi yote.

Utoaji Wa Leseni Waongezeka
Waziri Mavunde amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya leseni 12,130 zilitolewa sawa na asilimia 117.8 ya lengo la mwaka 2024/25. Kati ya Julai na Desemba 2025 pekee leseni 8,418 zilitolewa, sawa na asilimia 147 ya lengo la kipindi hicho.

Aidha,amesema leseni 73 zilifutwa baada ya kubainika kutokuendelezwa, maeneo hayo yakitarajiwa kutengwa kwa wachimbaji wadogo, vijana na wanawake kupitia programu ya MBT.

Biashara Ya Madini Yaongezeka Nchini
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ilisajili masoko 44 na vituo 114 vya ununuzi wa madini, ambapo biashara ya Sh trilioni 4.031 ilifanyika. Kati ya Julai – Desemba 2025 biashara ya Sh trilioni 3.102 ilifanyika kupitia masoko hayo.

Maabara Za Kisasa Zaongezewa Nguvu
Mhe.Mavunde amsema wizara imeanza ujenzi wa maabara kubwa ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini Kizota, Dodoma, yenye thamani ya Sh bilioni 14.3. Sambamba na hilo, ujenzi wa maabara za kanda Chunya na Geita unaendelea, huku sampuli 19,705 zikichambuliwa kati ya Julai – Desemba 2025.

Minada Ya Vito Yaleta Mapato
Waziri amesema minada mitatu ya vito iliyofanyika Mirerani na Arusha imeingiza madini yenye thamani ya Sh bilioni 2.74, huku Serikali ikipata zaidi ya Sh milioni 247 kupitia ada mbalimbali. Wizara pia inaandaa kurejesha Arusha Gem Fair (AGF) ifanyike kila mwaka.

Nishati Safi Ya Kupikia Yaendelea Kusogezwa Kwa Wananchi
Pia Waziri Mavunde amesema kuwa wizara imenunua mitambo miwili ya kuzalisha Rafiki Briquettes inayosimikwa Tabora na Dodoma, itakayokamilika Februari – Machi 2026. Pia imegawa makontena 10 katika mikoa mbalimbali na kukamilisha ununuzi wa pikipiki 30 zitakazokabidhiwa mawakala Februari 2026.

Utafiti Wa Madini Waongezewa Kasi
Serikali imetekeleza utafiti katika QDS 221 na 222 Rufiji na Kibiti, na kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti hadi asilimia 98. Aidha, vituo 32 vya kufuatilia matetemeko ya ardhi vimesimikwa, hatua inayoongeza usalama katika shughuli za madini.

About the author

mzalendo