| Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao kazi cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu – FIU, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma. |
Na. Joseph Mahumi na Saidina Msangi, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu wa Kuzuia Utakasishaji Fedha Haramu ambaye pia ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, pamoja na Kamishna wa FIU, Bw. Majaba Magana.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri wa Fedha, jijini Dodoma, pande hizo zimejadili masuala mbalimbali yanayohusu udhibiti wa utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi, sambamba na mikakati mipya ya kidigitali inayolenga kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa vitendo hivyo.
Waziri wa Fedha amepongeza jitihada za FIU na wadau wengine katika kuhakikisha mifumo ya udhibiti wa fedha haramu inaendelea kuimarika nchini, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi zote zinazohusika katika sekta ya fedha na usalama wa Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu wa Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu ambaye pia ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo, alisema kuwa Tanzania itakua mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Ubadilishaji wa Taarifa za Udhibiti wa Fedha Haramu Duniani (EGMONT Group meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 26 hadi 30 Januari 2026, jijini Arusha.
Vilevile, katika kikao hicho, walizungumzia mafanikio ya Tanzania kuondolewa kwenye Orodha ya Nchi zenye Mapungufu ya Kimkakati katika mifumo ya kudhibiti utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi (Grey List) mwezi Juni mwaka jana, hatua ambayo imeongeza imani ya kimataifa kwa mfumo wa fedha wa Tanzania.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula (Mb), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na FIU.




