Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, amefanya ziara katika Gereza la Mahabusu Mkoani Morogoro tarehe 5 Januari, 2026 kwa lengo la kufuatilia na kujionea namna haki inavyotekelezwa kwa watu wanaoshikiliwa katika maeneo ya vizuizi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kunakuwepo mazingira rafiki yanayozingatia misingi ya haki katika maeneo ya vizuizi, hatua inayolenga kulinda haki za wanaoshikiliwa na kuimarisha utawala wa sheria nchini.
Amepongeza jeshi la Magereza kwa kuendelea na programu za urekebu kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi mahabusu na wafungwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi pindi watakaporejea katika jamii.
Aidha, kuhusu matumizi ya teknolojia, Dkt. Homera amesema Serikali itaendelea kuyapatia magereza vifaa vya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, usimamizi wa magereza na mifumo ya haki jinai kwa ujumla.
Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kupunguza idadi ya mahabusu na wafungwa magerezani kwa kuimarisha mifumo ya haki, kuharakisha usikilizwaji wa mashauri, pamoja na kupanua matumizi ya adhabu mbadala.