Featured Kitaifa

MABASI 30 YA UDART KUREJEA BARABARANI, HUDUMA KUFIKA MLOGANZILA – PROF. SHEMDOE

Written by Alex Sonna

Na James Mwanamyoto – Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amefanya ziara ya ukaguzi katika karakana ya UDART eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, ili kujionea hatua za ukarabati wa mabasi yaendayo haraka yaliyokuwa yamepata hitilafu.

Katika ziara hiyo leo Januari 06, 2026 Prof. Shemdoe amesema, Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilitoa Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya kununua vipuri muhimu ikiwemo injini ili kufufua mabasi yaliyokuwa yamesitisha huduma.

Prof. Shemdoe amesema kupitia fedha hizo, jumla ya mabasi 30 yanatarajiwa kurejea barabarani, ambapo tayari mabasi 17 yamekamilika na yako tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Serikali iliona ni muhimu kuyarejesha mabasi haya barabarani. Ndio maana ilitoa fedha kwa ajili ununuzi wa vipuri na injini, na kati ya mabasi 30 tunayotarajia kuyarejesha, tayari 17 yamekamilika na yako tayari kuanza kazi,” amefafanua Prof. Shemdoe.

Aidha, Waziri Shemdoe amemuagiza Mkurugenzi wa UDART Bw. Pius Ngindo, kuhakikisha kuwa kuanzia kesho mabasi yaendayo haraka yaanze kufika Hospitali ya Mloganzila, ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na wagonjwa wanaofuata huduma za matibabu katika hospitali hiyo.

“Wapo wananchi wanaopata shida kufika Mloganzila. Ni muhimu tukapanua huduma na kuhakikisha mabasi yanafika huko ili kurahisisha safari za wagonjwa na ndugu zao,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Akizungumza kuhusu uboreshaji wa mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema Serikali imetoa Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya ununuzi wa mabasi mapya 99 yaendayo haraka.
Prof. Shemdoe ameeleza kuwa kati ya mabasi hayo, tayari 49 yamewasili bandarini na taratibu zinaendelea ili yakamilishe usajili na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam.
“Muda si mrefu mabasi haya mapya yataanza kazi, na yataleta nafuu kubwa ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameahidi kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata tabasamu kupitia huduma ya usafiri wa uhakika, salama na nafuu.

About the author

Alex Sonna